Uchaguzi wa Rais wa Tunisia na changamoto zake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56000-uchaguzi_wa_rais_wa_tunisia_na_changamoto_zake
Wananchi wa Tunisia kesho Jumapili wataelekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa mapema kumchagua rais wao wa baadaye miongoni mwa wagombea 26 wa kiti hicho ikiwa zimepita siku 50 tangu kuaga dunia Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 14, 2019 11:35 UTC
  • Uchaguzi wa Rais wa Tunisia na changamoto zake

Wananchi wa Tunisia kesho Jumapili wataelekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa mapema kumchagua rais wao wa baadaye miongoni mwa wagombea 26 wa kiti hicho ikiwa zimepita siku 50 tangu kuaga dunia Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia.

Watunisia wanaoishi nje ya nchi walianza kupiga kura zao katika uchaguzi huo jana Ijumaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa, vituo 391 vya kupigia kura vimeainishwa katika majimbo 310 ya uchaguzi, maeneo sita yakiwa nje ya Tunisia.

Uchaguzi wa Rais wa Tunisia ulikuwa umepangwa kufanyika Novemba 17 mwaka huu. Hata hivyo kifo cha Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo kimepelekea uchaguzi huo ufanyike mapema. Yusuf Chahid Waziri Mkuu aliyejiuzulu, rais wa zamani wa Tunisia Moncef al Marzouq, Abdelkarim  Zbidi Waziri wa Ulinzi na Nabeel al Qaroui tajiri na mmiliki wa televisheni binafsi ya "Nessma" wanatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushaindi katika uchaguzi huo. Pamoja na hayo kutiwa mbaroni al Qaroui kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji fedha kumezusha mjadala na gumzo kubwa nchini Tunisia. Maafisa wa vyombo vya mahakama wa Tunisia wanamtambua tajiri huyo kuwa ni mhalifu japokuwa yeye mwenyewe anadai kuwa baadhi ya wagombea wa kiti cha urais Tunisia wamekula njama ya kumfanya ashindwe. Vilevile amekanusha madai hayo akisema kesi hiyo imechochewa na malengo ya kisiasa.

Wafuasi wa mmiliki huyo wa vyombo vya habari wanawatuhumu wapinzani wake wenye nguvu na madaraka kwamba wanajaribu kumnyamazisha na kusitisha kampeni yake inayokosoa sera za serikali na hali mbaya ya uchumi.

 Nabil Karoui

Uchaguzi wa Rais Tunisia unafanyika katika hali ambayo masuala ya kupambana na ufisadi, kulinda uhuru na kujitawala wka nchi hiyo, kutatua matatizo ya kiuchumi, kuleta ustawi wa kijamii na kisiasa, kutekeleza uadilifu na kurejesha usalama yanahesabiwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoshughulisha zaidi fikra za Watunisia. Kuhusiana na suala hilo, vita dhidi ya ufisadi imekuwa changamoto kuu kiasi kwamba, akthari ya wagombea wa uchaguzi wa sasa wa rais wanasisisiza udharura wa kupambana na tatizo hilo.

Weledi wa mambo kwa upande wao wanaamini kuwa, tatizo la ufisadi limeshtadi zaidi baada ya Januari 14 mwaka 2011 (siku ya ushindi wa harakati ya wananchi huko Tunisia). Mbunge na wakili Mohamed Abbou anasema: "Katika kipindi cha utawala wa Zine El-Abidine Ben, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ulikuwa ukifanywa na familia ya dikteta huyo, lakini sasa ufisadi huo unafanyika kwa kutumia mwavuli wa demokrasia." 

Mohamed Abbou

Suala la uchumi pia ni miongoni mwa mambo yaliyotawala kampeni za uchaguzi wa rais nchini Tunisia. Takwimu zinaonesha kuwa, ukosefu wa ajira baina ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 umefikia asilimia 30, kiwango ambacho ni mara mbili ya wastani wa ukosefu wa ajira. Vilevile ughali wa maisha umekuwa mara mbili zaidi ya ule ulioshuhudiwa nchini humo katikati ya miaka ya 90, kwa kadiri kwamba, familia watu maskini haziwezi kumudu gharama za kununua chakula cha kila siku, gesi, umeme na kadhalika.

Katika upande mwingine mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi yamevuruga amani na usalama wa nchi hiyo, suala ambalo limepelekea kupungua idadi ya watalii wa kigeni. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, sekta ya utalii ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya pato la taifa nchini Tunisia. Kwa msingi huo wagombea wote katika uchaguzi wa kesho wameahidi kuboresha uchumi na kustawisha sekta ya utalii.

Alaa kulli hal, uchaguzi wa sasa wa rais wa Tunisia unafanyika katika wingu lenye giza na Watunisia wengi wana wasiwasi kuhusiana na mustakbali wa nchi yao na taathira mbaya za uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Kwa kadiri kwamba, hata baadhi ya wagombea katika uchaguzi wa kesho wameeleza wasiwasi wao kuhusiana na uingiliaji kati wa nchi kama Saudi Arabia na Imarati katika masuala ya ndani ya Tunisia. Kwa mfano tu siku chache zilizopita rais wa zamani nchi hiyo Moncef el Marzouki aliitaka Saudi Arabia ikome kuingilia masuala ya ndani ya Tunisia. Vilevile Hamadi Jebali ambaye ni miongoni mwa wagombea katika uchaguzi wa kesho nchini Tunisia amesema kuwa: "Imarati inaingilia uchaguzi wa nchi yetu na inawafadhili baadhi ya wagombea kwa shabaha ya kulitwisha taifa mtu anayetakiwa na Abu Dhabi."

Hamadi Jebali

Uchaguzi wa kesho wa rais nchini Tunisia ni mtihani mwingine mkubwa wa demokrasia na jinsi ya kulinda matunda ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 ambayo yaliuondoa madarakani utawala wa kidekteta wa Zine El-Abidine Ben. Hivyo, suala la kulindwa matunda hayo ya wananchi wa Tunisia linahesabiwa kuwa na umuhimu mkubwa zaidi bila ya kujali nani ataibuka mshindi katika kinyang'anyiro hicho.