Wananchi Tunisia washiriki katika uchaguzi ulio mgumu kutabiri mshindi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56020-wananchi_tunisia_washiriki_katika_uchaguzi_ulio_mgumu_kutabiri_mshindi
Wananchi wa Tunisia leo wameshiriki katika uchaguzi wa rais ambao wataalamu wa mambo wanasema kuwa ni vigumu sana kutabiri mshindi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2019 07:54 UTC
  • Wananchi Tunisia washiriki katika uchaguzi ulio mgumu kutabiri mshindi

Wananchi wa Tunisia leo wameshiriki katika uchaguzi wa rais ambao wataalamu wa mambo wanasema kuwa ni vigumu sana kutabiri mshindi.

Huo ni uchaguzi wa pili huru wa rais tangu wananchi wa Tunisia walipompindua dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo, Zine el Abidine Ben Ali mwaka 2011.

Uchaguzi huu umefanyika kabla ya wakati wake kufuatia kifo cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Beji Caid Essebsi aliyetawala Tunisia tangu mwaka 2014. Essebsi alifariki dunia tarehe 25 Julai mwaka huu wa 2019 akiwa na umri wa miaka 92. Hii ni katika hali ambayo mjane wa rais huyo wa zamani, Bi Chadlia Saïda Farhat naye amefariki dunia leo Jumapili, Julai 15, 2019 kwa mshituko wa moyo akiwa na umri wa miaka 83 yaani mwezi mmoja tu tangu alipofariki dunia mumewe.

Watu wamejitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi wa Tunisia

Zaidi ya wananchi milioni 7 wa Tunisia wametimiza masharti ya kupiga kura. Wagombea 24 wamejitokeza katika kinyang'ang'anyiro hicho cha uchaguzi wa rais.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tunisia, mshindi wa uchaguzi huo lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura. Hata hivyo kati ya wagombea wote 24 hakuna hata mmoja mwenye uungaji mkubwa wa wananchi wa kumuwezesha kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa uchaguzi huo kuingia duru ya pili.

Marehemu Beji Caid Essebsi na mkewe, marehemu Chadlia Saïda Farhat

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa mbili asubuhi leo. Baadhi ya vituo vimefungwa mapema kutokana na sababu za kiusalama. Awali wagombea walikuwa 26, lakini wagombea wawili wamejitoa dakika za mwisho kwa faida ya Waziri wa Ulinzi Abdelkarim Zbidi muda mchache kabla ya kumalizika muda wa kampeni za uchaguzi jana Jumamosi.