Uchaguzi wa rais nchini Tunisia waingia duru ya pili
Matokeo ya awali ya kura zilizohesabiwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika jana Jumapili nchini Tunisia, yanaonyesha kwamba kinyume na utabiri wa hapo awali, kiongozi wa chama kisicho mashuhuri na mgombea wa chama cha kujitegemea, wameonekana kuingia duru ya pili ya uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa matokeo ya kura zilizohesabiwa mpaka sasa, Kaïs Saïed, mgombea wa kujitegemea, amepata asilimia 19 ya kura huku Nabil Karoui wa chama cha 'Qalbu Tunis' akipata asilimia 15 ya kura na hivyo kuingia duru ya pili ya uchaguzi. Abdelfattah Mourou, mgombea wa chama cha al-Nahdhah ameshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 11 ya kura. Kabla ya uchaguzi, Kaïs Saïed, mgombea wa kujitegemea hakuwa mtu mashuhuri, kama ambavyo mpinzani wake Nabil Karoui naye bado anaendelea kuzuiliwa jela kwa kesi ya ufisadi na utakatishaji fedha.
Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia na ambaye pia ni mmoja wa wagombea, amekubali kushindwa katika uchaguzi huo. Tume ya Uchaguzi nchini humo sambamba na kutoa matokeo ya awali, imesema kuwa kiwango cha ushiriki katika uchaguzi wa jana kiliwa cha asilimia 45, ambapo jumla ya wagombea 24 walichuana vikali katika uchaguzi huo. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Tunisia, duru ya pili ya uchaguzi wa rais inatakiwa kufanyika katika kipindi cha wiki mbili tangu kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa duru ya kwanza.