Uchaguzi wa Tunisia na mustakbali usiojulikana wa nchi hiyo
Wananchi wa Tunisia juzi Jumapili, Septemba 15, 2019 walishiriki kwenye uchaguzi muhimu sana wa Rais ambao ulikuwa wa pili huru baada ya wananchi hao kumpindua dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo, Zine el Abidine Ben Ali mwaka 2011.
Uchaguzi huo uliowashirikisha wagombea 24 umefanyika kwa usalama na amani. Matokeo ya awali yameonesha kwamba, wagombea wawili Kaïs Saïed, wa kujitegemea, na Nabil Karoui wa chama cha 'Qalb Tounes' ndio walioingia duru ya pili ya uchaguzi huo kwa kupata asilimia kubwa zaidi ya kura ikilinganishwa na wagombea wengine.
Uchaguzi wa rais nchini Tunisia ulikuwa ufanyike tarehe 17 Novemba mwaka huu wa 2019, lakini imebidi ufanyike kabla ya wakati wake kufuatia kifo cha Beji Caid Essebsi rais wa zamani aliyetawala Tunisia tangu mwaka 2014. Essebsi alifariki dunia tarehe 25 Julai mwaka huu wa 2019 akiwa na umri wa miaka 92. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kujitokeza idadi kubwa ya wagombea kwenye uchaguzi huo wa juzi Jumapili ni ishara ya kuanza kuota mizizi na kuimarika misingi ya demokrasia nchini Tunisia. Wataalamu mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa Sayansi Jamii wanaona kuwa ni jambo lililo mbali kutokea machafuko na kukanyagwa misingi ya demokrasia nchini Tunisia.
Wataalamu hao wa mambo walitabiri mapema pia kwamba uchaguzi wa rais wa Jumapili, Septemba 15, 2019 huko Tunisia ungeliingia kwenye duru ya pili kutokana na kwamba, wagombea wote 24 hawakuwa na idadi ya kutosha ya wafuasi wa kuwawezesha kupata zaidi ya silimia 50 ya kura. Baadhi ya wachambuzi walitabiri kuwa Yusuf al Shahid, waziri mkuu wa hivi sasa wa Tunisia alikuwa na nafasi kubwa ya kupata kura nyingi zaidi akifuatiwa na Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia. Mwengine aliyekuwa amepewa nafasi ya kupata kura nyingi ni Waziri wa Ulinzi Abdelkarim Zbidi na Abdelfattah Mourou wa chama cha al-Nahdhah ambaye katika matokeo ya awali ameshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 11 ya kura. Awali wagombea walikuwa 26, lakini wagombea wawili walijitoa dakika za mwisho kwa faida ya Waziri wa Ulinzi Abdelkarim Zbidi yaani muda mchache kabla ya kumalizika wakati wa kampeni za uchaguzi siku ya Jumamosi.
Hata hivyo kama tulivyotangulia kusema, matokeo ya awali ya uchaguzi huo yamebatilisha utabiri wote huo kwani ni Kaïs Saïed, mgombea wa kujitegemea ndiye aliyeongozwa kwa kupata asilimia 19 ya kura za matokeo hayo ya awali akifuatiwa na Nabil Karoui wa chama cha 'Qalb Tounes' aliyepata asilimia 15. Wagombea hao wawili ndio walioingia katika duru ya pili ya uchaguzi huo. Nabil Karoui ni mmiliki wa kituo maarufu cha televisheni cha Nasma. Hivi karibuni alitiwa mbaroni na kushikiliwa korokoroni kwa tuhuma za kutakatisha fedha. Hata hivyo Tume ya Uchaguzi ya Tunisia iliruhusu aendelee kugombea kutokana na kwamba sheria ya uchaguzi haikumzuia kugombea, kama ambavyo pia hakuna hukumu ya mahakama iliyokuwa imetolewa dhidi yake. Mgombea huyo ameanza mgomo wa kula kulalamikia kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.
Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia na ambaye kama tulivyotangulia kusema, alikuwa miongoni mwa wagombea waliotabiriwa kupata kura nyingi, ametangaza rasmi kukubali kushindwa kwenye uchaguzi huo. Wakati ikitangaza matokeo ya awali ya uchaguzi huo, Tume ya Uchaguzi ya Tunisia imesema, asilimia 45 ya wapiga kura wamejitokeza kwenye kinyang'anyiro hicho. Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Tunisia, duru ya pili ya uchaguzi wa rais inatakiwa kufanyika katika kipindi cha wiki mbili tangu kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa duru ya kwanza.
Amma moja ya wasiwasi mkubwa wa wananchi wa Tunisia ambao cheche ya maandamano makubwa ya wananchi ilianzia nchini mwao na kuenea katika ulimwengu mzima wa Kiarabu na kupelekea hadi sasa kuangushwa viongozi wa Tunisia, Algeria, Misri, Libya, Sudan na Yemen, ulikuwa ni kuimarika misingi ya demokrasia nchini mwao na kutoruhusu kurejea mfumo wa kidikteta. Mijadala ya uchaguzi iliyofanyika nchini humo imeonesha kuwa demokrasia imeanza kukita mizizi huko Tunisia.
Hatua ya Moncef Marzouki, rais wa zamani wa Tunisia kuwa mwepesi wa kukubali kushindwa ni ishara nyingine nzuri ya kuonesha uvumilivu wa kisiasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hata hivyo baadhi ya wataalamu wanasema kuwa, mapinduzi ya wananchi wa Tunisia yameshindwa kuzaa matunda ya kiuchumi na maisha bora yaliyotarajiwa na wananchi hasa kutokana na kwamba, kulalamikia hali mbaya ya maisha ndiyo iliyokuwa cheche ya mapinduzi ya wananchi hao mwaka 2011 yaliyomng'oa madarakani dikteta Zine el Abidine Ben Ali.