Mgombea urais aliyeko jela Tunisia ataka uchaguzi uahirishwe
-
Nabil Karoui
Mwenyekiti wa chama cha Qalb Tunes anayefungwa jela ambaye amefanikiwa kuingia duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ametoa wito wa kuahirishwa zoezi hilo.
Nabil Karoui ameashiria kuendelea kushikiliwa kwake gerezani na kushindwa kushiriki katika kampeni za uchaguzi na ametaka uchaguzi wa rais ujao nchini humo uakhirishwe.
Hata hivyo Kamisheni ya Uchaguzi ya Tunisia imekataa wito huo na kutangaza kuwa, uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 13 mwezi huu wa Oktoba.
Nabil Karoui ameitaka kamisheni hiyo imruhusu kutembelea mikoa yote 24 ya Tunisia na kuzungumza moja kwa moja na wananchi katika kampeni za uchaguzi.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Tunisia uliofanyika tarehe 17 Septemba, mgombea wa chama cha Kiislamu cha al Nahdha Kaïs Saïed alipata asilimia 18.4 ya kura akifuatiwa na mgombea wa chama cha Qalb Tunes, Nabil Karoui ambaye alipata asilimia 15.58 ya kura.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tunisia, chama kinachofanikiwa kupata viti vingi bungeni ndicho kinachopewa jukumu la kuunda serikali kwa kura na idhini ya Bunge katika kipindi kisichozidi miezi miwili.
Uchaguzi wa rais wa Tunisia ambao awali ulipangwa kufanyika tarehe 17 Novemba ulifanyika mapema zaidi kutokana na kufariki dunia aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Beji Caid Essebsi. Essebsi alifariki dunia tarehe 25 Julai mwaka huu wa 2019 akiwa na umri wa miaka 92.
Huo ni uchaguzi wa pili huru wa rais tangu wananchi wa Tunisia walipompindua dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo, Zine el Abidine Ben Ali mwaka 2011.