Duru ya pili ya uchaguzi wa rais Tunisia imefanyika leo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56597-duru_ya_pili_ya_uchaguzi_wa_rais_tunisia_imefanyika_leo
Wananchi wa Tunisia mapema leo wameelekea katika masanduku ya kupigia kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais uliowashindanisha tajiri na mmiliki wa televisheni binafsi ya "Nessma" Nabeel Karoui na Wakili Mhafidhina, Kais Saied.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 13, 2019 12:14 UTC
  • Duru ya pili ya uchaguzi wa rais Tunisia imefanyika leo

Wananchi wa Tunisia mapema leo wameelekea katika masanduku ya kupigia kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais uliowashindanisha tajiri na mmiliki wa televisheni binafsi ya "Nessma" Nabeel Karoui na Wakili Mhafidhina, Kais Saied.

Wagombea hao waliojipambanua kama wagombea wa nje waliibua mshangao katika siasa za Tunisia wakati walipoibuka kidedea miongoni mwa wagombea wengine 26 wa kiti cha urais wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika Septemba 15 mwaka huu.

Katika duru hiyo ya kwanza, Saied alipata asilimia 18.4 ya kura huku Karoui akishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 15.6 ya kura. Wagombea hao wawili wa duru ya pili ya uchaguzi wa Rais Tunisia Ijumaa mchana walishuhudiwa katika maidani kuu katika mji mkuu Tunis wakinadi sera zao katika dakika za mwisho za kumalizika kampeni zao. Nebeel Karoui alisisitiza katika mkutano wake huo wa kampeni kuhusu kukomesha umaskini na kuongeza kuwa, anataka kuongeza madaraka ya rais kwa kupanua maana ya neno usalama wa taifa; akisema kuwa anataka lijumuishwe na masuala ya kijamii na uchumi wa nchi.

Wagombea wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais Tunisia
 

Hiyo ni moja ya hotuba chache za wazi mbele ya wananchi kutolewa na Karoui katika kampeni zake tangu atiwe nguvuni na kufungwa jela mwezi Agosti kwa tuhuma za kutakatisha pesa na kukwepa kulipa kodi. Karoui amekanusha tuhuma hizo akisema kuwa zimechochewa kwa malengo ya kisiasa.