Bunge la Tunisia lamjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56746-bunge_la_tunisia_lamjibu_waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_bahrain
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Nje katika Bunge la Tunisia amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain kuwa, uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo umeonyesha kuwa wananchi wa nchi hiyo wameamua kujiainishia wenyewe mwenendo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2019 08:56 UTC
  • Bunge la Tunisia lamjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Nje katika Bunge la Tunisia amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain kuwa, uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo umeonyesha kuwa wananchi wa nchi hiyo wameamua kujiainishia wenyewe mwenendo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Latif Habashi amejibu matamshi ya Khalid bin Hamad Al Khalifa Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain aliyedai kuwa Qatar ilikuwa na nafasi kubwa katika mchakato wa uchaguzi wa Tunisia kwa kusema: Tunisia haiiruhusu nchi yoyote kuingilia masuala yake ya ndani; na baada ya uchaguzi huo wa karibuni, Tunisia imesisitiza kuhusu siasa zake hizo kuliko jambo jingine lolote. 

Matokeo ya uchaguzi wa bunge la Tunisia umezikasirisha nchi za Saudi Arabia na Imarati na kumpelekea Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain kudai kuwa, Qatar imehusika pakubwa kwenye mchakato wa uchaguzi huo. Chama cha Kiislamu cha An Nahdha kilishinda uchaguzi wa bunge wa Tunisia kwa kupata viti 52 vya uwakilishi bungeni kati ya jumla ya viti 217 na sasa kinajiandaa kumuarifisha shakhsia mmoja kutoka chama hicho kuwa Waziri Mkuu atakayeunda serikali. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Nje katika Bunge la Tunisia pia amesema kutafanyika hafla ya kumuapisha rais mpya wa nchi hiyo. Amesema  Kais Saied ataapishwa bungeni tarehe 23 mwezi huu. 

Kais Saied, mshindi wa kiti cha rais Tunisia