Rais mpya wa Tunisia ala kiapo na kuanza rasmi kuiongoza nchi
Kais Saied, Rais mpya wa Tunisia aliyeshinda duru ya pili ya uchaguzi wa Rais iliyofanyika mwezi huu, leo ameapishwa na kuanza rasmi kuiongoza nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Sherehe za kuapishwa Rais Kais Saied zimefanyika katika ukumbi wa Bunge katika mji mkuu Tunis na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Rais Kais Saied ambaye ni profesa mstaafu wa sheria anakuwa Rais wa tatu wa Tunisia tangu yalipotokea mapinduzi ya umma nchini humo.
Duru ya pili ya uchaguzi wa Rais nchini Tunisia ilifanyika Jumapili ya tarehe 13 mwezi huu na matokeo yasiyo rasmi yalionyesha kuwa, mgombea wa Kais Saied ambayye alishiriki kkama mgombea wa kujitegemea aliibuka na ushindi kwa kujipatia asilimia 75 ya kura.
Kais aliibuka na ushindi katika hali ambayo, alikataa kujiunga na mrengo na chama chochote cha kisiasa katika kampeni za uchaguzi na hata alikataa kupokea ruzuku ya serikali inayotolewa kwa wagombea.
Pamoja na hayo, Kais Saied alipata himaya na uungaji mkono wa Chama cha Kiislamu cha al-Nahdha ambacho kimeibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge.
Uchaguzi hu9o wa kabla ya wakati nchini Tunisia ulifanyika baada ya kufariki dunia aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Beji Caid Essebsi Julai 25 mwaka huu. Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, miongoni mwa changamoto anazokabiliwa nazo Rais mpya wa Tunisia ni ufisadi uliokita mizizi katika nchi hiyo.