Wananchi wa Tunisia waandamana kulaani udhalilishaji wa kijinsia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57606-wananchi_wa_tunisia_waandamana_kulaani_udhalilishaji_wa_kijinsia
Mamia ya wananchi wa Tunisia wameshiriki kwenye maandamano ya kulaani udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na kuwataka viongozi wa nchi hiyo kulinda haki za tabaka hilo la wananchi linalokandamizwa katika jamii.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 01, 2019 03:41 UTC
  • Wananchi wa Tunisia waandamana kulaani udhalilishaji wa kijinsia

Mamia ya wananchi wa Tunisia wameshiriki kwenye maandamano ya kulaani udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na kuwataka viongozi wa nchi hiyo kulinda haki za tabaka hilo la wananchi linalokandamizwa katika jamii.

Shirika la habari la AFP limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wananchi hao wamefanya maandamano hayo baada ya kuenea picha zisizo za kimaadili za mbunge mmoja mpya wa Tunisia anayejulikana kwa jina la Zouheir Makhlouf kwa chama cha Qalb Tunes.

Hata hivyo mbunge huyo amekanusha madai yote yaliyotolewa dhidi yake, lakini kukanusha huko hakukuzuia wimbi la maandamano yanayotaka apokonywe ubunge kwa udhalilishaji wa kijinsia. Kampeni dhidi ya mbunge huyo inaendeshwa chini ya Hashtag ya #EnaZeda yenye maana "Mimi Vile Vile" kwa Kiarabu cha Tunisia.

Maandamano ya harakati ya #EnaZeda nchini Tunisia

 

Mwezi Oktoba mwaka huu, mwanafunzi mmoja wa kike alilalamika kuwa amedhalilishwa na mbunge huyo, madai ambayo yamekanushwa na bunge huyo.

Waandamanaji hao pia wanataka elimu ya raia iongezwe nchini Tunisia ili kupunguza udhalilishaji na unyanyasaji wa wanawake katika vyombo vya usafiri wa umma na maeneo mengineyo.

Kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa mwezi Julai 2017 na Bunge la Tunisia, ni kinyume cha sheria kufanya udhalilishaji wowote wa kijinsia katika maeneo ya umma na atakayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na fidia ya dola elfu moja. 

Hata hivyo sheria hiyo haijazuia vitendo hivyo nchini Tunisia na hadi hivi sasa wanawake wanaendelea kulalamikia kudhalilisha kijinsia mabarabarani. na kwenye maeneo ya umma.