Vyama viwili Tunisia vyakataa kujiunga na serikali ya Waziri Mkuu mteule
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57720-vyama_viwili_tunisia_vyakataa_kujiunga_na_serikali_ya_waziri_mkuu_mteule
Vyama vikuu viwili nchini Tunisia vimesema kuwa havitajiunga na serikali ya Waziri Mkuu mteule wa nchi hiyo Habib Jemli; hatua inayomaanisha kuwa serikali yoyote ya mseto itakayoundwa nchini humo itayumba na hivyo kuzidisha hatari ya kuibuka mgogoro wa kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2019 23:18 UTC
  • Vyama viwili Tunisia vyakataa kujiunga na serikali ya Waziri Mkuu mteule

Vyama vikuu viwili nchini Tunisia vimesema kuwa havitajiunga na serikali ya Waziri Mkuu mteule wa nchi hiyo Habib Jemli; hatua inayomaanisha kuwa serikali yoyote ya mseto itakayoundwa nchini humo itayumba na hivyo kuzidisha hatari ya kuibuka mgogoro wa kisiasa.

Vyama vya Achaab na Attayar vimechukua uamuzi huo baada ya wiki kadhaa za mazungumzo baada ya Tunisia kuendesha uchaguzi mwezi Oktoba mwaka huu; uchaguzi ulioligawanya pakubwa bunge la nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, hakuna chama kilichoshinda zaidi ya robo ya viti vya uwakilishi bungeni katika uchaguzi huo tajwa.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita Habib Jemli alisema kuwa anataraji kuunda serikali wiki ijayo na kwamba wanasiasa wa kujitegemea watapewa nyadhifa muhimu katika serikali hiyo ya mseto. Taarifa ya chama cha Achaab imeeleza kuwa, aina hii ya uundaji serikali haionyeshi azma na utambulisho wowote wa serikali mpya. Chama hicho kimesema kuwa, hakiko tayari kushiriki katika serikali ya Waziri Mkuu mteule Habib Jemli.

Naye Mohamed Abbou mkuu wa chama cha Attayar amesema kuwa chama hicho hakitajiunga na serikali hiyo mpya ya Tunisia wala kuiunga mkono katika  kura ya kuwa na imani nayo baada ya Jemli kukataa kukipatia chama hicho wizara za Mambo ya Ndani na Sheria. Tunisia sasa inahitaji serikali yenye nguvu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali kama maandamano ya wananchi yanayosababishwa na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, hali ngumu ya maisha na kuwepo haja ya kutekelezwa marebisho ya kimsingi nchini humo.

Mohamed Abbou, Mkuu wa chama cha Atyayar cha nchini Tunisia