Wanigeria waandamana kupinga uingiliaji wa mambo ya ndani wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57788-wanigeria_waandamana_kupinga_uingiliaji_wa_mambo_ya_ndani_wa_ufaransa
Wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano nje ya ubalozi mdogo wa Ufaransa mjini Lagos, kupinga na kulalamikia hatua ya Paris ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Dec 10, 2019 04:29 UTC
  • Wanigeria waandamana kupinga uingiliaji wa mambo ya ndani wa Ufaransa

Wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano nje ya ubalozi mdogo wa Ufaransa mjini Lagos, kupinga na kulalamikia hatua ya Paris ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Waandamanaji hao wakiwemo maveterani chini ya vuguvugu la Harakati ya Ukombozi Afrika wameikosoa vikali serikali ya Rais Emmanuel Macron wanayoituhumu kuwa inaingilia masuala ya ndani ya Nigeria, mbali na kuyauzia silaha makundi ya kigaidi kama Boko Haram.

Wamesema kitendo hicho cha nchi hiyo ya Ulaya cha kuyauzia silaha magenge ya kigaidi sio kwa maslahi ya nchi hiyo au nchi yoyote ile ya Afrika.

Waandamanaji hao wameipa serikali ya Paris wiki tatu kukomesha mwenendo wake huo wa kudhalilisha uhuru wa kujitawala Nigeria.

Wanachama wa Boko Haram wakiwa na silaha zao kutoka Magharibi

Taarifa ya waandamanaji hao imesisitiza kuwa, Ufaransa inaunga mkono ugaidi katika bara la Afrika, kwa kuyauzia silaha makundi ya kigaidi.

Ingawa serikali ya Paris imekuwa ikikanusha madai hayo ya kuunga mkono ugaidi barani Afrika, lakini kutolewa picha iliyoonesha helikopta ya Ufaransa katika ngome ya Boko Haram nchini Cameroon kuliipa nguvu dhana hiyo kuwa Paris inaunga mkono ugaidi barani Afrika.