Waasi wa Nigeria waua wanajeshi 20 na kufanya uharibifu mkubwa
Askari wasiopungua 20 wa jeshi la Nigeria wameuawa na watu wengine karibu elfu moja wamelazimika kukimbia makazi yao baada ya waasi kushambulia mji mmoja ulioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti zinasema waasi hao walivamia mji wa Monguno katika jimbo la Borno mapema jana na kushambulia wanajeshi wa serikali. Vilevile wameharibu nyumba zisizopungua 750 za raia wa mji huo.
Mkazi wa mji wa Monguno, Gumati Sadu amesema raia wengi wamekimbilia msituni kuokoa uhai wao na kwamba wenzao watatu wameuawa katika mapigano yaliyozuka baina ya askari usalama na wanamgambo hao.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amekataa kutoa maelezo yoyote kuhusiana na hujuma hiyo.
Kundi lenye mfungamano na magaidi wa Daesh limetangaza kuwa ndilo lililohusika na hujuma hiyo.
Kundi hilo linalojiita ISWAP lilijitenga na kundi la kigaidi la Boko Haram mwaka 2016 na limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Nigeria.
Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka imetahadharisha kuwa maelfu ya raia wa eneo la Monguno waliokimbia makazi yao kutokana na hujuma za makundi hayo ya kigaidi hawana makazi, maji safi ya kunywa na huduma za afya.