Rais wa Mali: Serikali iko tayari kuzungumza na makundi ya kigaidi
Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali amesema serikali yake iko tayari kukutana na kufanya mazungumzo na makundi ya kigaidi kwa shabaha ya kumaliza jinamizi la ugaidi ambalo mbali na kuchochea mapigano ya kikabila, pia limeifanya nchi hiyo ishindwe kutawalika na kustawi.
Rais Keita amesema hayo katika mahojiano na Idhaa ya Kimataifa ya Ufaransa na kueleza bayana kuwa, kushtadi mashambulizi dhidi ya maafisa usalama na raia kaskazini na katikati mwa Mali kumeifanya serikali ya Bamako iangalie upya mahesabu yake. Amehoji kwa kusema, "kwa nini tusitafute njia ya mawasiliano na wale ambao wanaendesha harakati hizo?"
Rais wa Mali amesisitiza kuwa, wakati umefika wa kutumia majukwaa mengine kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa ukosefu wa usalama na uthabiti katika nchi hiyo na eneo la Sahel la Afrika kwa ujumla.
Keita amebainisha kuwa, amempa jukumu Dioncounda Traore, rais wa zamani wa nchi hiyo ambaye ni mwakilishi mkuu wa serikali yake katika eneo la katikati mwa Mali, kuwasikiliza watu wote.
Makundi yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) yanaendesha harakati zao za kigaidi katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Mali na yamekuwa yakitumia maeneo hayo kama vituo vya kuratibia mashambulio yao dhidi ya askari na raia katika nchi jirani hasa Burkina Faso.
Harakati hizo za magenge ya kigaidi zinashuhudiwa nchini Mali licha ya Ufaransa kujipenyeza nchini humo kwa kutuma maelfu ya wanajeshi wake, mbali na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutuma pia kikosi cha askari wa kulinda amani nchini humo kinachojulikana kama MINUSMA.