Makundi yenye silaha yaendelea kumwaga damu Nigeria
Watu waliojizatiti kwa silaha wameshambulia jimbo la Delta kusini mwa Nigeria na kuua watu 10. Mashuhuda wanasema waliotekeleza ukatili huo walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya jimbo la Delta, Olisa Ifejika amesema kuwa kikosi cha jeshi kimetumwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuimarisha usalama.
Vyombo vya habari nchini Nigeria vimeripoti kuwa, watu hao walioendesha shambulizi hilo walikuwa na silaha huku wakiwa wamevalia sare za jeshi. Watu wengine wengi wameripotiwa kujeruhi katika shambulizi hilo.
Hakuna kundi lililotangaza kuhusika katika hujuma hiyo ya jana. Hata hivyo kundi la wanamgambo linalojiita Walipizaji Kisasi wa Delta (Delta Avengers) limekuwa likiendesha harakati zake za kigaidi na uasi katika eneo hilo la kusini mwa Nigeria
Jimbo la Delta la kusini mwa Nigeria lina utajiri wa mafuta na limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya magenge ya kigaidi na waasi.
Wanamgambo wa Delta Avengers walihusika na wimbi la mashambulio na machafuko yaliyoshuhudiwa mwaka 2016 ambayo yalichangia kuzorota kwa uchumi wa Nigeria.