Umoja wa Mataifa walaani jaribio la kumuua waziri mkuu wa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59670-umoja_wa_mataifa_walaani_jaribio_la_kumuua_waziri_mkuu_wa_sudan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali jaribio la kumuua Waziri Mkuu wa Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2020 01:17 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani jaribio la kumuua waziri mkuu wa Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali jaribio la kumuua Waziri Mkuu wa Sudan.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, akiwaarifu wanahabari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York amesema, Katibu Mkuu wa umoja huo António Guterres ameshitushwa na kusikitishwa baada ya kusikia habari ya shambulizi hilo na akaeleza kwamba yuko pamoja na Waziri Mkuu na watu wa Sudan.

Pia ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani jimboni Darfur, UNAMID umetoa taarifa ukieleza masikitiko yake kuhusu jaribio hilo la mauaji.

Hamdok aliteuliwa kuongoza serikali ya mpito mnamo mwezi Agosti baada ya kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir kuondolewa madarakani na majeshi kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya kuuupinga utawala wake.

Hali baada ya jaribio la kumuua Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok. Machi 9, 2020 Khartoum Sudan

Vyombo vya habari viliripoti kuwa shambulio lilitokea Jumatatu baada ya bomu kupiga gari la Waziri Mkuu huyo lakini hakuna aliyejeruhiwa.

Vyombo hivyo vya habari vimenukuu mashuhuda wa tukio hilo wakisema kuwa shambulio hilo lilitokea karibu na kaskazini mashariki mwa mwanzo wa daraja la Kober, ambalo linaunganisha kaskazini ya Khartoum na mjini, eneo ambalo waziri mkuu anaishi.