The Guardian: Imarati imempatia Haftari tani 5,000 za silaha
Ripoti iliyoandikwa na gazeti la Guardian la Uingereza imefichua kuwa, nchi ya Umoja wa Falme wa Kiarabu (Imarati) imempatia jenerali mstaafu wa Libya, Khalifa Haftar tani elfu tano za silaha tangu mwezi Januari mwaka huu.
Likitegemea takwimu za mfumo wa safari za anga, gazeti hilo limeripoti kuwa, Imarati imesafirisha silaha hizo kwa safari zaidi ya mia moja za ndege kutoka kwenye kambi za jeshi za nchi hiyo na kuelekea Libya au kutoka kwenye kambi ya jeshi inayosimamiwa na nchi hiyo huko Eritrea.
Ripoti ya The Guardian imefichua kuwa, usafirishaji wa shehena za silaha hizo ulikuwa ukifanyika kwa kutumia ndege za kuajiri zinazotua katika uwanja wa ndege uliopo karibu na Benghazi, ngome kuu ya Haftar, au huko magharibi mwa Misri, na kupuuza vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya makundi hasimu ya Libya.
Ripoti hiyo imesema shehena hizo za silaha zilijumuisha zana za teknolojia ya mawasiliano, aina mbalimbali za ilaha nzito na nyepesi, vipuri muhimu na kadhalika.
Mwezi Disemba mwaka uliopita gazeti hilo la Uingereza lilifichua kuwa, mamluki elfu tatu kutoka Sudan walikuwa wamewasili katika mji wa Benghazi kwa ajili ya kupigana katika safu za jenerali Khalifa Haftar na kwamba walijiunga na mamluki wengine 600 kutoka Russia.
Jenerali muasi Khalifa Haftari anapigana dhidi ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.