Uturuki: UAE inataka kuchochea uasi dhidi ya serikali za Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameutuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa unapania kuchochea harakati za uasi dhidi ya serikali katika nchi za Afrika.
Mevlüt Çavuşoğlu amesema Uturuki inapinga vikali njama za Imarati za kuzusha wimbi la uasi katika nchi za Afrika sanjari na kuigawa vipande vipande nchi ya Yemen.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uturuki ameashiria kuhusu nafasi ya UAE katika vita vya Libya na kueleza bayana kuwa, "iwapo mamlaka ya kujitawala ya Libya itahujumiwa, nchi zinazoizunguka ikiwemo Misri na Tunisia zitaathika vibaya pia."
Çavuşoğlu amebainisha kuwa, Imarati inafanya jitihada za kusababisha mpasuko na mgawanyiko Yemen, na kuchochea wimbi la uasi dhidi ya serikali zilizoko mamlakani katika nchi za Afrika na Kiarabu.
Mwezi uliopita wa Mei, Mwakilishi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) katika Umoja wa Mataifa, Taher Al-Sunni alisema: Umoja wa Falme za Kiarabu unakiuka sheria za kimataifa kwa kutuma silaha nchini Libya.
Alisema ana ushahidi kadhaa unaoonyesha kuwa Imarati imekiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwasaidia na kuwaunga mkono waasi nchini Libya na kuwapelekea silaha na zana za kijeshi.
Hivi karibuni pia, GNA ilisema watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu ndio wanaosababisha maafa nchini Libya kutokana na wanamgambo wake walioko chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar kutumia gesi za sumu katika mashambulizi yao.