Umoja wa Mataifa walaani hujuma dhidi ya askari wake CAR
Umoja wa Mataifa umelaani vikali hujuma iliyofanywa dhidi ya askari wake wa kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo imepelekea kuuawa askari mmoja wa kulinda amani raia wa Rwanda na wengine wawili kujeruhiwa.
Kikosi cha Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MUNISCA) kimetoa ripoti na kusema hujuma hiyo imetekelezwa na kundi la waasi linalojulikana kama Return, Reclamation, Rehabilitation, kwa kifupi 3R katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
MINUSCA imesema shambulizi hilo ni ukiukwaji wa mapatano ya amani na kundli hilo pamoja na kiongozi wake, Abass Sidiki. Kundi hilo la 3R ni kati ya makundi yaliyotia saini mapatano ya amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu zake za rambi rambi kwa familia ya askari aliyeuawa, na pia kwa watu na serikali ya Rwanda. Amesema mashambulizi dhidi ya askari wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuhesabiwa kuwa ni jinai za kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Guterres pia ametoa wito kwa wakuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchukua hatua za kuwakamatwa wahusika na kuwapandisha kizimbani.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013 baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.
Kwa sasa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajitahidi kurejesha utulivu katika nchi hiyo ya kati kati mwa Afrika.