Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yatangaza kusitisha vita
Wakati pande mbalimbali zikiendelea kulumbana juu ya namna ya kugawana keki ya Libya na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo, Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli imetoa amri ya kusitishwa vita mara moja na kusimamishwa operesheni zote za kijeshi.
Tangazo hilo limesema kuwa, lengo la kusitishwa vita ni kuiwezesha serikali kuwa na mamlaka kamili katika ardhi yote ya Libya na kuondoka vibaraka na vikosi vyote vya wapiganaji wa kigeni katika ardhi ya Libya. Tangazo hilo limesisitiza kuwa, ili kufanikisha usitisha vita huo, hapana budi kukusanywa silaha zote katika miji miwili ya Sirte na al Jufra. Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya pia imetaka kufanyike chaguzi za rais na bunge mwezi Machi mwaka 2021 kwa mujibu wa katiba itakayoungwa mkono na makundi yote.
Hatua hiyo ya kusitishwa vita imekubaliwa pia na serikali ya mashariki mwa Libya. Awali Aquila Saleh, Spika wa Bunge lenye makao yake katika mji wa Tobruk huko mashariki mwa Libya ambalo linamuungamkono jenerali muasi, Khalifa Haftar, alikuwa tayari ametoa wito wa kusitisha vita na kusimamishwa operesheni zote za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo. Ombi hilo lilikataliwa na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa kutokana na ukorofi na vizingiti vya wapiganaji wa Haftar.

Tangazo hilo la kusitishwa vita limetolewa huku madola ya kigeni na pande zinazozozana nchini Libya zikiendelea kufanya mazungumzo kuhusiana na hali ya nchi hiyo. Nchi za Ulaya zina wasiwasi kuhusu mustakbali wa Libya kutokana na nchi hiyo kukaribia mipaka ya Ulaya na hatari ya kuongezeka harakati za kigaidi nchini Libya. Wakai huo huo nchi hizo za Ulaya zinakodolea macho utajiri wa mafuta na maliasili za Libya. Kwa msingi huo kila moja kati ya nchi za Ulaya imekuwa ikifanya harakati za siri na mahusiano ya nyuma ya pazia na pande hasimu za Libya ingawa kidhahiri zinajivika "gwanda la ubinadamu" kwa kusisitiza udharura wa kudumishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya na umuhimu wa kutatuliwa mzozo wa ndani wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa.
Pamoja na hayo yote hali ya mambo nchini Libya inaripotiwa kuwa ni tata sasa. Hatua ya Uturuki ya kutuma wanamgambo elfu 30 nchini Libya na tangazo la kukaribia mashambulizi dhidi ya mji wa Sirte kwa ajili ya kuukomboa kikamilifu viliikasirisha Misri ambayo imeamua kutuma majeshi yake karibu na mpaka wa Libya na kutahadharisha kuwa, mji huo ni mstari mwekundu ambao haupaswi kuvukwa. Katika uwanja huo Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri ametangaza kuwa, iwapo Uturuki itatuma majeshi katika mji wa Sirte, Cairo itawasaidia wapiganaji wa Haftari kwa majeshi ya anga, nchi kavu na baharini.

Miji ya Sirte na al Jufra inahesabiwa kuwa maeneo muhimu sana katika mapigano ya ndani ya Libya kwa kadiri kwamba inasemekana kuwa iwapo Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa itafanikiwa kutwaa maeneo hayo itakuwa kama iimepata ushindi kamili katika vita vya ndani vya nchi hiyo.
Hata hivyo inaonekana kuwa, mapigano zaidi yanaweza kuitumbukiza Libya katika vita vya pande zote na kuifanya kama Syria au Afghanistan ya Afrika.
Katika hali kama hii tangazo la kusitisha vita la pande mbili hasimu limehuisha matumaini ya kupatikana suluhisho la kisiasa la mzozo wa ndani wa Libya na ndiyo maana limepongezwa na nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa.
Hata hivyo tajiriba ya miaka iliyopita inaonesha kuwa, utajiri wa mafuta na nishati umekuwa na nafasi muhimu katika kuzichochea nchi za kigeni zinazokodolea macho utajiri huo. Vilevile ushindani wa nchi ajnabi wa kutaka kudhibiti utajiri huo na kuwa na ushawishi katika masuala ya ndani ya Libya ni iongoni mwa sababu kuu za ghasia na machafuko ya ndani ya nchi hiyo.
Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Abdel Barr Atwan anasema: Si ajabu kuona kwamba, mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini Mala yakawa mwanzo; hatua ya Rais Macron wa Ufransa ya kuzichochea nchi za Ulaya dhidi ya Uturuki ikawa utangulizi wa vita vya kieneo na labda vya kimataifa ambavyo ni vigumu sana kuweza kutabiri matokeo yake."