Sep 06, 2020 07:39 UTC
  • Askari wengine wa Ufaransa wauawa na kujeruhiwa nchini Mali

Wanajeshi wawili wa Ufaransa wameuawa huku mwingine mmoja akijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi huko kaskazini mwa Mali.

Hayo yametangazwa na Ofisi ya Rais wa Ufaransa ambayo imesema, askari hao waliuawa baada ya gari lao la deraya kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini katika eneo la Tessalit, kaskazini mwa Mali.

Wanajeshi hao wa Ufaransa waliouawa walikuwa sehemu ya vikosi vinavyoendesha Operesheni ya Barkhane yenye lengo la kutokomeza makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewapongeza wanajeshi wa Ufaransa walioko katika eneo hilo eti kwa kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya vita dhidi ya ugaidi, huku akitoa mwito wa kuundwa haraka iwezekanavyo serikali ya mpito ya kiraia nchini Mali.

Wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali

Ifahamike kuwa, maeneo ya kaskazini na katikati mwa Mali yamekumbwa na machafuko kutokana na kuweko huko magenge ya kigaidi yenye uhusiano na mitandao ya kigaidi ya al Qaida na Daesh (ISIS) ambayo mara kwa mara yanafanya mashambulio na mauaji ya kutisha dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali.

Hivi sasa mkoloni mkongwe wa Ulaya yaani Ufaransa ana wanajeshi 5,100 katika eneo hilo la Sahel Afrika lakini machafuko yanaendelea, bali hata yamekuwa makubwa zaidi, suala ambalo linawafanya wachambuzi wa mambo waamini kuwa, wanajeshi wa Ufaransa hawako katika eneo hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wala kwa ajili ya kupambana na magenge ya kigaidi, bali yako huko kwa ajili tu ya kulinda maslahi ya kikoloni ya Ufaransa.

Tags