Juhudi za Ufaransa za kutaka kuhalalisha uwepo wa majeshi yake nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63274-juhudi_za_ufaransa_za_kutaka_kuhalalisha_uwepo_wa_majeshi_yake_nchini_mali
Hali ya mambo nchini Mali inaripotiwa kuwa mbaya baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomlazimisha rais wa nchi hiyo kung'atuka madarakani.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Sep 07, 2020 05:50 UTC
  • Juhudi za Ufaransa za kutaka kuhalalisha uwepo wa majeshi yake nchini Mali

Hali ya mambo nchini Mali inaripotiwa kuwa mbaya baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomlazimisha rais wa nchi hiyo kung'atuka madarakani.

Mgogoro wa kisiasa uliotokea nchini humo umewapa wanajeshi fursa ya kung'ang'ania madaraka ya nchi na kufungua milango kwa nchi za kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Mali. Sasa Ufaransa imezidisha idadi ya wanajeshi wake katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian anadai kwamba, wanajeshi wa nchi hiyo wataendelea kuwepo nchini Mali kwa shabaha ya kulinda usalama wa Ufaransa! Le Drian ambaye anajaribu kupunguza athari mbaya za kuuliwa wanajeshi kadhaa wa Ufaransa nchini Mali amesisitiza kuwa, Paris haipasi kupunguza idadi ya wanajeshi wake nchini Mali. 

Mali inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi muhimu za Afrika kwa kutilia maanani jiografia ya kisiasa ya nchi hiyo na utajiri wake wa maliasili. Utajiri wa madini kama ya uranium, phosphate, boksiti na almasi na vilevile nafasi ya kijiografia ya nchi hiyo barani Afrika na kupakana kwake na nchi kama Algeria, Niger, na Ivory Coast vinaifanya Mali kuwa na umuhimu mkubwa kwa nchi za Magharibi hususan Ufaransa. Ufaransa iliimarisha zaidi uwepo wake nchini Mali mwaka 2013 kufuatia mgogoro wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo. Viongozi wa Ufaransa walitumia suala la kuisaidia Mali kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu nchini humo kama kisingizio cha kutuma maelfu ya wanajeshi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Katika miaka ya karibuni pia kushadidi harakati za makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali kumeipa Ufaransa kisingizio cha kutuma wanajeshi zaidi katika nchi ya Mali katika fremu ya operesheni iliyopewa jina la Barkhane.  

Waafrika wanawaona wanajeshi wa kigeni kama wavamizi

Katika fremu hiyo, zaidi ya wanajeshi 4,500 wa Ufaransa walitumwa katika eneo la Sahel barani Afrika kwa ajili ya eti kukabiliana na makundi ya kigaidi na yale yenye misimamo ya kufurutu mipaka. Wanajeshi hao walitazamiwa kuungana na wenzao kutoka nchi za Mali, Burkina Faso, Niger, Mauritania na Chad kwa ajili ya kupambana na makundi hayo. Hata hivyo inasikitisha kuwa, licha ya madai hayo hali bado si shwari katika eneo la Sahel, na harakati za makundi ya kigaidi katika kanda hiyo zimeshamiri zaidi. Wakati huo huo maafisa wa Ufaransa wametumia operesheni hiyo ya Barkhane kama kisingizio cha kuomba msaada wa kifedha kwa nchi za Ulaya waitifaki wa nchi hiyo na hata Marekani.

Katika upande mwingine utendaji wa Ufaransa katika nchi hizo umezusha malalamiko mengi ya wananchi. Waafrika wanasema Wafaransa wanataka kuzidisha ushawishi wao barani humo katika kalibu ya ukoloni mambo leo. Louis Magloire Komayou ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Afrika anasema: "Waafrika wamepoteza matumaini yao kwa askari wa kigeni. Kuwepo kwa muda mrefu wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali kumewafanya raia wa nchi hiyo wawatambue kuwa ni askari vamizi."

Askari wa Ufaransa eneo la Sahel

Alaa kulli hali, kuondolewa madarakani Ibrahim Boubacar Keita katika mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 18 mwezi Agosti kumezidisha hali ya ukosefu wa amani nchini Mali na kudhoofisha operesheni ya kukabiliana na makundi ya waasi na magaidi wa al Qaida na Daesh katika kanda ya Sahel. Suala hilo linazidisha wasiwasi nchini humo na katika eneo la magharibi mwa Afrika kwa ujumla. Halii hii inatumiwa vibaya ya nchi za Magharibi hususan Ufaransa kwa ajili ya kuingia masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo.

Inaonekana kuwa, Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi zinataka kudumisha ukoloni wao katika nchi za Afrika lakini kwa kutumia mbinu mpya na za kisasa kama madai ya kulinda demokrasia, kuimarisha amani, haki za binadamu na kadhalika.