EACJ yatupilia mbali faili la ukomo wa urais nchini Uganda
Mahakama ya Uadilifu ya Afrika Mashariki (EACJ) imetupilia mbali faili lililowasilishwa kwake la kupinga uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Uganda, wa kuidhinisha mabadiliko ya katiba yalioondoa ukomo wa umri wa kugombea urais katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Akisoma hukumu hiyo hii leo kwa niaba ya majaji watano wa mahakama hiyo, Jaji Mwandamizi Monica Mugenyi amesema uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Uganda wa kuidhinisha mabadiliko ya katiba yalioondoa ukomo wa umri wa kugombea urais katika nchi hiyo wa miaka 75, haukukiuka sheria za Uganda.
Kadhalika mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha Tanzania imemtenga Jaji Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe na tuhuma zilizowasilishwa dhidi yake katika korti hiyo. Aliyewasilisha kesi hiyo katika mahakama hiyo ya EACJ alimtuhumu Katureebe kuwa ni jaji asiye na uadilifu, anayeegemea upande mmoja na asiye na ujuzi na ufahamu wa masuala ya sheria.
Aidha EACJ imemtaka wakili mashuhuri wa Uganda, Hassan Male Mabirizi ambaye aliwasilisha faili hilo katika mahakama hiyo ya kikanda afidie gharama za kesi hiyo baada ya kushindwa kwake.
Uamuzi wa leo kwa ujumla umeunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Uganda wa Aprili mwaka jana 2019, ulioidhinisha marekebisho ya katiba ya kuondoa kipengee chenye kuweka ukomo wa umri wa miaka 75 kwa mgombea wa kiti cha urais.
Uamuzi huo ulimpa Rais Yoweri Museveni ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986 na mwenye umri wa miaka 75, nafasi ya kuwania tena kiti hicho mwaka 2021 na kuendelea hadi mwaka 2026.