Umoja wa Afrika warejesha uanachama wa Mali baada ya ECOWAS kufuta vikwazo
(last modified Fri, 09 Oct 2020 12:39:39 GMT )
Oct 09, 2020 12:39 UTC
  • Umoja wa Afrika warejesha uanachama wa Mali baada ya ECOWAS kufuta vikwazo

Umoja wa Afrika Ijumaa ya leo umetangaza kurejesha uanachama wa nchi ya magharibi mwa Afrika ya Mali uliosimamishwa baada ya wanajeshi wa nchi hiyo kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo mwezi Agosti mwaka huu.

Uamuzi huo umechukuliwa siku tatu baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) kufuta vikwazo ilivyoweka dhidi ya Mali baada ya mapinduzi ya kijeshi, ikitaka kurudisha utawala wa kiraia nchini humo.

Vikwazo hivyo vilijumuisha kufungwa mipaka, marufuku ya biashara ya na mabadilishano ya kifedha yasiyohusu mahitaji ya kimsingi kama dawa, vifaa vya kupambana na virusi vya corona, mafuta na umeme.

Assimi Goita, kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Mali

Taarifa iliyotolewa mapema leo na AU imesema: "Kwa kutilia maanani maendeleo mazuri ya karibuni katika masuala ya kisiasa, Baraza la Amani na Usalama, limeamua kuondoa marufuku ambayo ilikuwa imewekwa dhidi ya Mali."

Serikali ya mpito ya Mali inayoongozwa na Rais Bah N'daw na Waziri Mkuu Moctar Ouane iliapishwa mwezi uliopita na itaendelea kuongoza nchi kwa kipindi cha miezi 18.

Tags