Wanasiasa Libya wapinga kuanzishwa uhusiano kati ya nchi hiyo na Tel Aviv
Duru za kidiplomasia nchini Tunisia zimeripoti kuwa, aghalabu ya wanasiasa na wanajeshi wa Libya wanapinga kuanzishwa uhusiano kati ya Tripoli na Tel Aviv.
Duru hizo zimeripoti kuwa, nukta ya pamoja kati ya aghalabu ya wanasiasa na makamanda wa kijeshi katika maidani za vita huko Libya ni upinzani wao kwa hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano kati ya Libya na utawala wa Kizayuni. Duru hizo za kidiplomasa za Tunisia zimeongeza kuwa, Walibya sawa kabisa na Tunisia na Algeria wanawaunga mkono wananchi wa Palestina; na taarifa yoyote kwamba Walibya wameafiki kuanzishwa uhusiano kati ya nchi yao na Tel Aviv si ya kweli. Duru hizo zimebainisha kuwa, taarifa kama hizi zinasambazwa kwa lengo la kuzichochea fikra za waliowengi na kupuuza mafanikio waliyopata Walibya kwenye mazungumzo ya kisiasa.
Wanadiplomasia wa Tunisia wamesema si jambo lililo mbali kutokea mapigano ya kijeshi huko Tripoli na kueleza kuwa, hitilafu baina ya baadhi ya makundi ya wanamgambo na wanasiasa katika mji mkuu Tripoli zimeongezeka sana kwa sababu, makundi ya wanamgambo wenye silaha yanapasa kupokonywa silaha kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa na kamati za mazungumzo kati ya pande za Libya.
Wanadiplomasia hao wameashiria pia kufanyika kikao cha mazungumzo ya kisiasa ya Libya mwezi ujao wa Novemba na kueleza kuwa serikali ya Algeria katika siku chache zijazo itakuwa mwenyeji wa kikao cha kiuchumi na kijamii cha makundi ya Walibya.