UN: Mazungumzo ya amani Libya yanaendelea kwa mafanikio huko Ghadames
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mazungumzo ya pande hasimu nchini Libya yanayoendelea katika mji wa Ghadames ulioko kusini magharibi mwa nchi hiyo yamepiga hatua kubwa katka njia ya kufikia makubaliano juu ya utekelezaji wa mapatano ya kusitisha vita yaliyotiwa saini wiki kadhaa zilizopita.
Tume ya kijeshi inayoshirikisha wawakilishi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na wapiganaji wa Khalifa Haftar ilianza mazungumzo jana katika mji wa Ghadames, na maudhui kuu ni njia ya utekelezaji wa mapatano ya Geneva yaliyofikiwa tarehe 23 Oktoba.
Mazungumzo hayo yatakayoendelea kwa kipindi cha siku tatu ambayo anasimamiwa na Umoja wa Mataifa ni ya kwanza kufanyika ndani ya ardhi ya Libya. Awali mazungumzo hayo yalifanyika katika miji ya Cairo na Geneva.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya, Stephanie Williams amesema mazungumzo hayo yamepiga hatua na kufikia maelewano. Hata hivyo Bi Stephanie Williams hakutoa maelezo zaidi.
Amesema kuwa pande hizo mbili leo Jumanne zinajadili jinsi ya kutekeleza vipengee vya makubaliano ya kusitisha vita.
Masuala mengine yanayojadiliwa ni pamoja na kuundwa tume ya kusimamia kundoka kwa majeshi ya pande mbili huko magharibi mwa mji wa Sirte, kukomesha uwepo wa wapiganaji mamluki katika ardhi ya Libya na kufunguliwa barabara za mashariki, magharibi na kusini mwa Libya.
Mazungumzo ya sasa ya kijshi baina ya pande mbili hasimu za Libya yatafuatiwa na mazungumzo mengine ya kisiasa yaliyopangwa kufanyika nchini Tunisia tarehe 9 mwezi huu wa Novemba. Umoja wa Mataifa unasema kuwa mazungumzo ya kisiasa ya Tunisia yatashirikisha wawakilishi wa utawala ulioondolewa madarakani nchini Libya.