Somalia yamtimua balozi wa Kenya na kumwita nyumbani balozi wake aliyeko Nairobi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64929-somalia_yamtimua_balozi_wa_kenya_na_kumwita_nyumbani_balozi_wake_aliyeko_nairobi
Somalia imemwita nyumbani balozi wake aliyeko Nairobi sambamba na kumpa masaa 24 balozi wa Kenya mjini Mogadishu awe ameondoka katika ardhi ya Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 30, 2020 08:06 UTC
  • Somalia yamtimua balozi wa Kenya na kumwita nyumbani balozi wake aliyeko Nairobi

Somalia imemwita nyumbani balozi wake aliyeko Nairobi sambamba na kumpa masaa 24 balozi wa Kenya mjini Mogadishu awe ameondoka katika ardhi ya Somalia.

Kutokana na kile kilichotajwa kama uingiliaji wa Kenya katika masuala ya kisiasa na kiuchumi ya Somalia, Serikali ya Shirikisho ya Somalia jana ilimwita nyumbani balozi wake wa nchini Kenya Mohamud Ahmed Nur Tarsan na kumtaka balozi wa Kenya nchini humo Lucas Tumbo arudi Nairobi kwa mashauriano.

Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia Mohamed Ali Nur amesema, uamuzi huo umechukuliwa kutokana na uingiliaji wa Kenya katika uchaguzi ujao wa eneo la Jubaland.

"Serikali imechukua uamuzi huu kulinda mamlaka yake ya kitaifa ya kujitawala baada ya kudhihirika kuwa Kenya inaingilia masuala ya Somalia, hususan ya Jubaland", imeeleza taarifa iliyotolewa na Nur.

Rais Ahmed Mohamed Islaam Madobe wa eneo la Jubaland

Somalia imeituhuma Kenya kwamba imekuwa ikimshinikiza sana rais wa Jubaland Ahmed Mohamed Islaam Madobe atekeleze mambo yenye maslahi kisiasa na kiuchumi kwa nchi hiyo na hivyo kudhoofisha makubaliano ya kisiasa yaliyosainiwa hivi karibuni nchini Somalia, ukiwa ni ukiukaji wa taratibu za kidiplomasia.

Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia amesisitiza kuwa Mogadishu haitakubaliana katu na kitendo chochote kile kinachodhoofisha usalama na mamlaka yake ya kujitawala.

Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, Mohamed Ali Nur amesema, kutokana na uingiliaji wa kisiasa wa Kenya katika masuala ya ndani ya Somalia, rais wa eneo la Jubaland amehalifu makubaliano yaliyosainiwa Septemba 17 mjini Mogadishu kuhusu uchaguzi wa eneo hilo.

Ameongeza kuwa inavyoamini Serikali ya Shirikisho ya Somalia, vitendo vinavyofanywa na serikali ya Kenya haviendani na mahusiano ya kidiplomasia yanayotambuliwa kimataifa na madola yanayojitawala.../