Somalia yawafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya, yawataka wake warudi nyumbani
Serikali ya Somalia imetangaza kusitisha uhusiano wake na Kenya ikidai kwamba Serikali ya Kenya inaingilia masuala yake ya ndani.
Nchi hiyo jirani wa Kenya, imetangaza kuwafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya na kuagiza wanadiplomasia wake wote walioko Nairobi warudi Mogadishu ndani ya siku saba kuanzia leo Jumanne Desemba 15, 2020.
Waziri wa Habari wa Somalia, Osman Abubakar Dubbe, amesema katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya serikali ya Somalia jana Jumatatu jioni kwamba hatua hiyo imechukuliwa kujibu uchokozi wa kisiasa wa kila mara unaofanywa na serikali ya Kenya kinyume na uhuru wa Somalia.
Hata hivyo Serikali ya Kenya haijajibu madai wala hatua hiyo ya Somalia.
Somalia ilimuondoa Balozi wake nchini Kenya Novemba 29 na kuamuru balozi wa Kenya kuondoka Mogadishu.
Wakati huo, Somalia iliishutumu Kenya kwa kuingilia masuala yake ya ndani na siasa za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa Novemba 29 na Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia, Mohamed Ali Nur, nchi hiyo ilichukua uamuzi huo kulinda mamlaka yake ya kitaifa ya kujitawala baada ya kudhihirika kuwa Kenya inaingilia masuala ya Somalia, hususan ya Jubaland.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba Kenya imekuwa ikimshinikiza sana rais wa Jubaland Ahmed Mohamed Islaam Madobe atekeleze mambo yenye maslahi kisiasa na kiuchumi kwa nchi hiyo na hivyo kudhoofisha makubaliano ya kisiasa yaliyosainiwa hivi karibuni nchini Somalia, ukiwa ni ukiukaji wa taratibu za kidiplomasia.
Kwa mujibu wa Serikali kuu ya Somalia, kutokana na uingiliaji wa kisiasa wa Kenya katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, rais wa eneo la Jubaland amehalifu makubaliano yaliyosainiwa Septemba 17 mjini Mogadishu kuhusu uchaguzi wa eneo hilo.../