9 wauawa katika mpaka wa Kenya na Somalia, AU yatoa kauli
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema amani katika mpaka wa Kenya na Somalia ni jambo muhimu kwa ajili ya uthabiti wa eneo zima la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.
Moussa Faki Mahamat amesema hayo leo Jumanne katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, anafuatilia kwa makini taharuki iliyotanda katika mpaka wa nchi mbili hizo.
Ametoa mwito kwa majirani hao kujizuia kuchukua hatua yoyote inayoweza kuzidisha hali ya taharuki, na kuzitaka serikali za Mogadishu na Nairobi kutafutia ufumbuzi mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo, kwa kufuata mchakato wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na Pembe ya Afrika (IGAD).
Kauli ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU imekuja baada ya watu tisa kuripotiwa kuuawa katika mji wa Bulohawo, jimbo la Jubaland mpakani mwa Kenya na Somalia.
Hapo jana serikali ya Somalia ilidai kuwa, wanamgambo waliojizatiti kwa silaha na wanaofadhiliwa na kuungwa mkono na serikali ya Kenya waliingia katika mji huo wa Somalia wakitokea Kenya na kuanzisha mapigano hayo. Waziri wa Habari wa Somalia, Osman Abukar Dube amesema wanajeshi watatu wa Somalia wameuawa katika mapigano hayo, mbali na watoto watano pamoja na mama yao.
Hata hivyo serikali ya Nairobi imekanusha tuhuma hizo, ikisisitiza kuwa imeweka maafisa usalama wa kutosha katika mpaka wake na Somalia kwa ajili ya kulinda doria.
Mwezi uliopita, Somalia ilitangaza kukata rasmi uhusiano wa kidiplomasia na Kenya na kuilaumu Kenya kwa kujaribu kuingilia mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.