Uganda yaishambulia EU kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66802-uganda_yaishambulia_eu_kwa_kuingilia_masuala_ya_ndani_ya_nchi_hiyo
Serikali ya Uganda imeukosoa vikali Umoja wa Ulaya kwa kile ilichodai kuwa ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2021 05:20 UTC
  • Uganda yaishambulia EU kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo

Serikali ya Uganda imeukosoa vikali Umoja wa Ulaya kwa kile ilichodai kuwa ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Hii ni baada ya Bunge la EU kupasisha azimio la kutaka kuwekewa vikwazo maafisa wa nchi hiyo, kwa kutumia mkono wa chuma kukandamiza na kuwakamata wapinzani wa Rais Yoweri Museveni kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita.

Aidha Bunge la Umoja wa Ulaya katika kikao cha Alkhamisi lilisema uchaguzi wa mwezi uliopita nchini Uganda haukuwa wa kidemokrasia, na kwamba askari polisi na wanajeshi wa nchi hiyo walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wapinzani, huku likitoa mwito wa kuachiwa huru wanachama wa upinzani.

Msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo amelihutubu Bunge la EU kwa kuliambia kuwa: Kutoa mwito wa kuachiwa huru washukiwa waliofikishwa mbele ya mahakama ni uingiliaji usiofaa wa mchakato halali  wa kisheria. Amesema serikali ya Kampala inalitazama azimio hilo la EU kuwa halina msingi wala uadilifu, na lengo lake hadi sasa halifahamiki.

Mwezi uliopita pia, Uganda iliikosoa vikali Marekani kwa kuingilia siasa zake za ndani, na kuitihumu kuwa inajaribu kudunisha na kudhalilisha mchakato wa uchaguzi wa urais wa Januari 14.

Wapigakura katika foleni ya kuwachagua viongozi Uganda mnamo Januari 14

Tume ya Uchaguzi Uganda ilimtangaza rasmi Yoweri Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa Januari 14, kwa kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote wakati mpinzani wake wa karibu,  Bobi Wine akipata kura milioni 3.48 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.

Mahakama ya Juu ya nchi hiyo inaendelea kusikiliza kesi ya Wine ya kupinga matokeo hayo yaliyomrejesha Museveni (76) madarakani kwa muhula wa sita.