Serikali: Wakenya milioni 1.4 wanasumbuliwa na njaa
(last modified Thu, 01 Apr 2021 12:09:39 GMT )
Apr 01, 2021 12:09 UTC
  • Serikali: Wakenya milioni 1.4 wanasumbuliwa na njaa

Msemaji wa serikali ya Kenya amesema kwa akali Wakenya milioni moja na laki nne wanasumbuliwa na njaa.

Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, Msemaji wa serikali ya Kenya amesema hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, yumkini idadi hiyo ikaongezeka katika siku zijazo iwapo hatua za dharura hazitachuliwa.

Amesema taifa hilo linawaomba washirika wake wa kimataifa kama Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Benki ya Dunia kuingilia kati ili kunusuru maisha ya mamilioni ya Wakenya wanaosumbuliwa na njaa.

Kanali Oguna amesema kaunti zilizoathirika zaidi na baa la njaa nchini humo ni Turkana, Mandera, Garissa, Wajir na Isiolo.

Kwa mujibu wa serikali ya Kenya, mbali na ukame na kiangazi, jambo jingine lililosababisha baa hilo la njaa na uhaba wa chakula katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ni vizingiti vinavyokwamisha kazi na biashara kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Licha ya baadhi ya maeneo ya Kenya kushuhudia kiangazi, mengine yanasumbuliwa na mafuriko

Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, asilimia 10 ya watu duniani ambayo ni sawa na watu milioni 821.6 duniani kote wanakabiliwa na baa la njaa.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO) yalitangaza hivi karibuni kuwa, njaa na lishe duni ni miongoni mwa sababu kuu za vifo na udhaifu wa kinga mwilini hususan barani Afrika.