May 08, 2021 12:18 UTC
  • Rwanda mbioni kuwa nchi ya kwanza Afrika kuzalisha chanjo ya Corona

Huku bara la Afrika likiendelea kukabiliwa na uhaba wa chanjo za Corona, Rwanda imesema inafanya mashauriano na kampuni kadhaa zinazotengeneza chanjo hizo, ili kuhakikisha zinaanza kuzalishwa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Dakta Tharcisse Mpunga, Waziri wa Serikali ya Rwanda anayesimamia huduma za msingi za afya amesema, nchi hiyo inafuatilia njia za kuhakikisha chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 inazalishwa nchini humo.

Amesema kuna matumaini kwamba, mazungumzo yanayoendelea kati ya Rwanda na washirika wake yatazaa matunda karibuni, na kwamba kuanza kuzalishwa chanjo nchini humo si tu kutaleta ahueni kwa nchi hiyo, bali kwa bara Afrika kwa ujumla.

Hivi karibuni pia, Rais Paul Kagame alisema Rwanda inafanya kazi na washirika wake ili kupeleka kampuni ya kwanza ya kuzalisha chanjo kwa kutumia mfumo wa mRNA barani Afrika.

Mwezi uliopita, viongozi wa nchi za Afrika walioshiriki Kongamano la Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Umoja wa Afrika (Afrika-CDC) lililojadili suala la uzalishaji wa chanjo za kukabiliana na virusi vya Corona; walisisitiza kuwa bara la Afrika linahitaji ujuzi na uwezo wa kujitengenezea chanjo za kupambana na ugonjwa wa Covid-19, wakati huu ambapo bara hilo linakumbwa na uhaba mkubwa wa chanjo hizo.

Roboti za kupambana na Corona nchini Rwanda

Rais Paul Kagame wa Rwanda aliliambia kongamano hilo kuwa, usawa katika ugavi wa chanjo za Corona hauwezi kudhaminiwa na irada njema tu, lakini bara Afrika linahitaji uwezo wa kujitengenezea chanjo na madawa yake.

Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa Mataifa (UN) kwa mara kadhaa zimekosoa ugawaji usio wa kiadilifu wa chanjo za Corona duniani. 

Tags