May 11, 2021 02:50 UTC
  • Afrika Kusini yasema nchi tajiri zinafanya 'apartheid ya chanjo' ya Corona

Rais wa Afrika Kusini ametahadharisha kuwa, iwapo nchi tajiri duniani zitaendelea kuhodhi chanjo za ugonjwa wa Covid-19, huku mamilioni ya watu katika nchi masikini wakiendelea kuaga dunia kwa kukosa chanjo hizo, kitendo hicho ni sawa na 'apartheid ya chanjo.'

Rais Cyril Ramaphosa aliyasema hayo jana Jumatatu na kusisitiza kuwa, chanjo inapaswa kuwa bidhaa ya umma duniani. Rais huyo wa Afrika Kusini kwa mara nyingine tena amekosoa ugawaji usio wa kiadilifu wa chanjo za Corona duniani.

Ameeleza bayana kuwa, "sinario ambapo idadi kubwa ya jamii za nchi zilizostawi duniani inapokea chanjo kwa njia salama, huku mamilioni ya watu katika nchi masikini duniani wakifariki dunia wakiwa katika foleni ya kusubiri chanjo hizo, ni sawa na (ubaguzi aina ya) apartheid (katika ugavi) wa chanjo."

Ramaphosa amesema Afrika Kusini ni katika nchi tano za bara Afrika zenye uwezo wa kuzalisha chanjo, na kwamba kuna haja ya kuwezeshwa na kuandaliwa mazingira ya kufanikisha hilo.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais huyo wa Afrika Kusini kulalamikia ugawaji usio wa kiadilifu wa chanjo za Corona duniani. Mwezi uliopita, alisema Afrika inahitaji ujuzi na uwezo wa kujitengenezea chanjo za kupambana na ugonjwa wa Covid-19, wakati huu ambapo bara hilo linakumbwa na uhaba mkubwa wa chanjo hizo.

Alisisitiza kuwa, "Bara Afrika linahitaji kukumbatia uwezo wake, na litambue fursa za ushirikiano miongoni mwa nchi za bara hilo ili lifanikiwe kujizalishia chanjo."

Tags