UN: Wanajeshi wa Kisomali wamehusika na mauaji ya kimbari ya Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71066-un_wanajeshi_wa_kisomali_wamehusika_na_mauaji_ya_kimbari_ya_tigray
Wanajeshi wa Somalia wanaopata mafunzo ya kijeshi nchini Eritrea wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya maelfu ya watu katika eneo la Tigray, huko kaskazini mwa Ethiopia.
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Jun 09, 2021 08:17 UTC
  • UN: Wanajeshi wa Kisomali wamehusika na mauaji ya kimbari ya Tigray

Wanajeshi wa Somalia wanaopata mafunzo ya kijeshi nchini Eritrea wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya maelfu ya watu katika eneo la Tigray, huko kaskazini mwa Ethiopia.

Ripoti maalumu ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu imesema, mamia ya wanajeshi wa Somalia waliokuwa wanapata mafunzo ya kijeshi nchini Eritrea, wamehusika na mapigano baina ya wanajeshi wa Ethiopia wakisaidiwa na wa Ertrea kwa upande mmoja, mkabala wa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

UN imesema ina ushahidi madhubuti wa kuhusika wanajeshi hao wa Kisomali katika mauaji ya mamia ya watu mwezi Novemba mwaka jana 2020 katika mji wa Axum eneo la Tigray linaloshuhudia mapigano kwa miezi kadhaa sasa.

Ethiopia ilitangaza hivi karibuni kuwa wanajeshi wa nchi jirani ya Eritrea wanaotuhumiwa kuua mamia ya raia wa Ethiopia wameanza kuondoka katika eneo linalokumbwa na mgogoro la Tigray lililo katika mpaka baina ya nchi hizo mbili za Afrika.

Mapigano katika eneo la Tigray

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana, kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray.