ICC yaitaka Uganda kueleza kwa nini haikumkamata Rais wa Sudan
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC imeitaka Uganda kueleza ni kwa nini ilishindwa kumkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipofanya ziara nchini humo wiki iliyopita.
Bashir alikuweko nchini Uganda kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Yoweri Museveni. Akizungumza katika sherehe za kuapishwa kwake, Rais Museveni alisema kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ni taasisi isiyo na maana na kudai kuwa ni mahakama ya watu wasio na maana.
Museveni aliyasema hayo baada ya kumuarifisha mbele ya hadhirina, Rais wa Sudan Omar el Bashir aliyekuwa miongoni mwa wageni waalikwa.
Kwa muda mrefu sasa mahakama hiyo, ICC imekuwa ikitaka Rais wa Sudan, Omar el Bashir kukamatwa baada ya kumfungulia mashtaka ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kutuma jeshi na kuwaunga mkono wanamgambo wa Kairabu kuzima uasi huko Darfur mwaka 2003.
ICC imetoa waranti wa kumkamata Rais al Bashir kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliotokea mkoani Darfur, nchini Sudan. Barua iliyoandikwa na ICC kwa serikali ya Uganda ni ishara nyingine ya baadhi ya nchi kukerwa na kauli zilizotolewa na rais Yoweri Museveni wa Uganda kuhusu mahakama hiyo.
Viongozi wa Afrika wamekuwa wakiilaumu ICC kuwa ni chombo cha madola ya kibeberu.