Watunisia waandamana dhidi ya serikali katika mji mkuu, Tunis
Wananchi wa Tunisia leo Jumapili wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis kupinga hatua za karibuni za Rais Kais Saeid.
Maelfu ya wananchi wa Tunisia leo walimiminika katika mji mkuu wa nchi hiyo dhidi ya Rais Kais Saeid kufuatia maamuzi yake ya karibuni. Washiriki katika maandamano wamemtaka Rais Saeid ajiuzulu na kuanza tena kazi za Bunge haraka iwezekanavyo. Vilevile wametaka kuheshimiwa Katiba ya nchi hiyo.
Maandamano hayo yamefanyika leo siku moja baada kujiuzulu zaidi ya viongozi 100 wa harakati ya Ennahdha ya Tunisia wakiwemo wabunge na wawakilishi wa Baraza la Ushauri la nchi hiyo.
Wanasiasa nchini Tunisia wamezitaja hatua za karibuni za Rais Kais Saed kuwa ni kuhodhi madaraka ya nchi na wakati huo huo wametahadharisha juu ya uwezekano wa Tunisia kurejea katika zama za udikteta.
Rais wa Tunisia tarehe 26 mwezi Julai mwaka huu alitoa dikrii na kumfuta kazi Waziri Mkuu, Hicham Mechichi, sambamba na kusimamisha shughuli za Bunge.
Aidha Rais wa Tunisia aliwaondolea wabunge kinga yao ya kisheria na kujilimbikizia mamlaka ya kuongoza nchi; hatua ambayo imetajwa na wapinzani nchini humo kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi ya serikali.