The Wall Street Journal: Uasi wa kiraia nchini Sudan unachochewa na hali mbaya ya uchumi
(last modified 2022-01-19T11:27:46+00:00 )
Jan 19, 2022 11:27 UTC
  • The Wall Street Journal: Uasi wa kiraia nchini Sudan unachochewa na hali mbaya ya uchumi

Gazeti la Kimarekani la "The Wall Street Journal" limeripoti kuwa uasi wa kiraia ulioanza jana Jumanne nchini Sudan unazidisha mzozo kati ya waandamanaji na majenerali wa jeshi la nchi hiyo.

Gazeti hilo limeripoti kuwa uasi wa kiraia ulioitishwa na makundi yanayotaka demokrasia, unaenda sambamba na mzozo wa kiuchumi unaochochea machafuko yaliyozuka baada ya mapinduzi ya kijeshi Oktoba mwaka jana.

Ripoti ya gazeti hilo imesema kwamba mapigano ya jana Jumatatu ambayo yamepelekea kuuawa waandamanaji 7 na mamia kujeruhiwa, yanachochea zaidi mvutano kati ya viongozi wa kijeshi waliofanya mapinduzi na vuguvugu la maandamano ya wananchi wakati juhudi za kidiplomasia za kukomesha machafuko ziendelea kulegalega. 

Viongozi wa vuguvugu la maandamano wanawashutumu majenerali wa jeshi la Sudan kuwa wamesimamia vibaya uchumi na kufuja mapato ya dhahabu na mafuta ya nchi hiyo.

Wakati huo huo, uchumi wa Sudan unaendelea kuporomoka kwa kasi na kiwango cha mfumuko wa bei kilipanda hadi asilimia 443 mwezi uliopita wa Disemba kutoka asilimia 163 mwaka 2020.sudan

Sudan

Uhaba wa bidhaa za kimsingi, kuanzia vyakula hadi dawa, unaendelea kuwakasirisha raia katika maeneo mengi nchini humo, suala linalotatiza juhudi za kukomesha makabiliano baina ya raia na watawala wa kijeshi nchini Sudani.

Jumuiya ya Madaktari wa Sudan iliripoti jana kuwa, polisi wa nchi hiyo wamewaua watu saba katika maandamano mapya dhidi ya utawala wa kijeshi nchini humo.

Jumuiya hiyo imeeleza kuwa hadi sasa watu 71 wameuawa katika ghasia na mapigano kati ya askari usalama na waandamanaji mjini Khartoum na katika miji mingine ya Sudan tangu baada ya mapinduzi ya Oktoba 25 mwaka jana.  

Tags