Feb 04, 2022 07:53 UTC
  • FAO yatoa wito wa kuwasaidia waathirika wa ukame katika nchi za Kenya, Ethiopia na Somalia

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO katika Ukanda wa Afrika Mashariki limetoa wito kwa wananchi, taasisi binafsi na mashirika ya dini kuchangia wananchi walioathirika na ukame pamoja na mazao yao kuharibiwa na nzige katika nchi za Kenya, Ethiopia na Somalia.

Dokta. Paul Mutungi, Afisa wa FAO anayehusika na wafugaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki amesema: “Hali ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika sio nzuri sana kwa sababu katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na baa la njaa ambalo limefuatiwa na janga la nzige na kisha janga la COVID-19."

Mutungi ameongeza kuwa, hata kabla ya janga la Covid-19 kuisha umekuja ukame mkali ambao umesababishwa na hali ya Ya-Nina na kuwaweka watu wengi sana hatarini kwa sababu kumekuwa na ukosefu wa chakula na kumekuwa na njaa, na sasa maisha ya watu hao yapo hatarini. 

Akitolea mfano wa maeneo yaliyoathirika na hali hiyo, afisa huyo wa FAO amesema, katika eneo la Mosobeti lililopo kusini mwa Kenya wafugaji na wanyama wengi sana wamekufa kwa sababu ya ukosefu wa lishe ya nyasi na hata maji; na kwamba watoto nao wamekuwa na utapiamlo. Maeneo mengine yaliyoashiriwa ni Turkana na Mandera ambako amesema kumeathirika sana.

Kwa mujibu wa FAO, katika nchi tatu za Kenya, Ethiopia na Somalia jumla ya watu milioni 25.3 wana uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa, watu hao wapo hatarini, na kwamba hali yao isipoangaliwa kufikia katikati ya mwaka huu (2022) maisha yao yatakuwa katika hatari kubwa sana.../ 

 

 

Tags