Waziri Mkuu wa Israel aitembelea Misri, akutana na Rais Sisi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81674-waziri_mkuu_wa_israel_aitembelea_misri_akutana_na_rais_sisi
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameripotiwa kuitembelea Misri katika ziara ya siri na kificho, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na ngazi za juu wa nchi hiyo, akiwemo Rais Abdel Fattah al-Sisi.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 22, 2022 22:12 UTC
  • Waziri Mkuu wa Israel aitembelea Misri, akutana na Rais Sisi

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameripotiwa kuitembelea Misri katika ziara ya siri na kificho, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na ngazi za juu wa nchi hiyo, akiwemo Rais Abdel Fattah al-Sisi.

Naftali Bennett alienda Cairo tangu juzi Jumatatu katika safari ya kushtukiza, ambayo haijatolewa maelezo na maafisa wa Misri na utawala haramu wa Israel.

Ziara hiyo imejiri baada ya tangazo la kuanza safari ya moja kwa moja ya ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu, hadi mji wa kitalii wa Misri wa Sharm el-Sheikh.

Duru za kidiplomasia zimedokeza kuwa, Sisi amekutana na Bennett pamoja na Mwanamfalme wa Abu Dhabi, Mohammed bin Zayed, katika kikao cha pande tatu cha Misri, Israel na Imarati kujadili 'masuala yenye maslahi ya pamoja ya usalama.'

Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa Israel kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Sisi wa Misri mwaka huu 2022.

Bennett aliitembelea Misri Septemba mwaka jana, katika ziara iliyokuwa ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa utawala pandikizi wa Israel katika nchi hiyo ya Kiarabu baada ya kupita muongo mmoja.

Hii ni katika hali ambayo, wanaharakati wa Misri wamekuwa wakionya kuwa, hatua ya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu kujipendekeza kwa utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yao ni tatizo kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu.