Russia yaanza ujenzi wa kituo cha kwanza cha nyuklia nchini Misri
Shirika la Taifa la Nishati ya Nyuklia la Russia ROSATOM limeanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo cha kwanza cha nyuklia nchini Misri.
Mamlaka ya Nishati ya Nyuklia ya Misri (EAEA) imesema ujenzi wa kituo hicho cha kuzalisha kawi ya nyuklia katika mji wa El Dabaa katika jimbo la Matrouh, yapata kilomita 300 kaskazini magharibi mwa Cairo, mji mkuu wa Misri ni mafanikio makubwa ya kistratajia kwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Uzinduzi wa kituo hicho cha kwanza kabisa cha nishati ya nyuklia nchini Misri umeongozwa na Alexei Likhachev, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Serikali ya Russia, na Mohammed Shaker, Waziri wa Umeme na Nishati Jadidika wa Misri.
ROSATOM ilipewa kibali cha kufanya mradi huo mnamo Juni 29, huku jiwe la msingi la kuanza ujenzi huo likiwekwa juzi Julai 20 mjini El Dabaa.
Serikali ya Misri ambayo itatumia takriban dola bilioni 25 katika utekelezaji wa mradi huo imesisitiza kuwa itaheshimu Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Usambajazi wa Silaha za Nyuklia wa NPT.
Ikumbukwe kuwa, Misri ilianzisha mradi wa nyuklia katika miaka ya 70 lakini ulisitishwa baada ya kutokea ajali kwenye kinu cha nyuklia cha Chernobyl cha Ukraine mwaka 1986.