Wananchi wa Burkina Faso waandamana dhidi ya Ufaransa
Mamia ya wananchi wa Burkina Faso wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu Ouagadougou kushiriki maandamano dhidi ya Ufaransa, hatua inayoonesha jinsi ushawishi wa Paris katika nchi za bara la Afrika unavyoendelea kupungua.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Reuters ambalo limeeleza kuwa, waandamanaji hao wa Burkina Faso wanaituhumu Paris kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kufanya ukoloni mamboleo.
Moja ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao mjini Ouagadougou jana Ijumaa lilikuwa limeandikwa "Ufaransa lazima iondoke.'
Aidha waandamanaji hao huku wakipiga nara wamesema Paris imeshindwa kutekeleza ahadi na majukumu yake katika mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo na ya kigaidi.
Burkina Faso ni koloni la zamani la Ufaransa, na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Ibrahim Traoré amekuwa akieleza wazi hisia zake dhidi ya Wafaransa tangu aingie madarakani, na amepanua uhusiano na nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Russia.
Mapema mwaka huu, Serikali ya Burkina Faso ilimtimua balozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou, Luc Hallade; hatua iliyochukuliwa katika kivumbi cha mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Hapo awali, serikali ya kijeshi ya Burkina Faso ilikuwa imetangaza katika taarifa yake kuwa imesitisha utangazaji wa Radio France Internationale (RFI) inayofadhiliwa na serikali ya Paris.
Sababu ya hatua hiyo ni kueneza taarifa za uongo, na kutangaza habari za upotoshaji. Uhusiano wa nchi kadhaa za Magharibi mwa Afrika na Ufaransa umeharibika sana katika miaka ya karibuni.