Jan 29, 2023 12:39 UTC
  • Ujerumani yakosolewa kwa ujumbe wa Twitter wa kuidhalilisha Afrika

Viongozi na watumiaji mitandao ya kijamii katika nchi za Afrika wameijia juu Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani kwa kuchapisha ujumbe wa dharau na kulidhalilisha bara hilo.

Ebba Kalondo, Msemaji wa Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ameashiria ujumbe huo wa udhalilishaji wa Ujerumani dhidi ya Afrika na kusema kuwa, nchi hiyo ya Ulaya imefanya makosa kwa kutaka kuisawiri Afrika kama bara ambalo halina kitu cha ziada isipokuwa wanyamapori.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani katika ujumbe huo uliochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter imemkejeli Waziri wa Mambo ya Russia, Sergei Lavrov kwa kufanya safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika karibuni. Imesema Lavrov hajafanya safari hiyo ya Afrika kwa ajili ya kwenda kutazama 'chui' bali ni kutaka eti kuhalalisha operesheni za Moscow dhidi ya Ukraine.

Kalondo amejibu ujumbe huo kwa kusema, hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani kutumia picha ya chui kwenye ujumbe wake ni kutaka kuionyesha Afrika kuwa ni bara la wanyamapori pekee. Amesema, sera za nje si suala la mzaha, na wala halipasi kutumiwa kwa ajili ya mashindano yasiyo na maana ya kijeopolitiki. 

Msemaji wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU amehoji kwa kuandika: Wakati bosi wako alipoutembelea Umoja wa Afrika wenye makao yake katika moja ya nchi 20 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na Ujerumani, je alikuja kutazama tu wanyama? Au bara Afrika, watu wake na wanyamapori ni dhihaka kwako? 

Lavrov alipoitembelea Afrika Kusini. Kabla ya hapo alienda Eswatini, Angola na Eritrea

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imetumia mchoro wa chui kwenye ujumbe huo baada ya Berlin hatimaye kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya waitifaki wake ikiwemo Marekani na kukubali kutuma Ukraine vifaru aina ya Leopard 2.

Akthari ya watumiaji wa mitandao ya kijamii barani Afrika wamelaani ujumbe huo wa udhalilishaji wa Wizara ya Mambo ya Ujerumani na kusisitiza kuwa, kejeli hizo ni muendelezo wa ukoloni mamboleo wa nchi za Ulaya kwa bara Afrika. 

 

Tags