AHAIC: Hakuna usalama wa afya duniani bila kujumuishwa Afrika
(last modified Tue, 07 Mar 2023 07:26:08 GMT )
Mar 07, 2023 07:26 UTC
  • AHAIC: Hakuna usalama wa afya duniani bila kujumuishwa Afrika

Viongozi wa sekta za afya Afrika wamesema dunia haitafanikiwa kuwa na usalama wa afya, iwapo nchi za bara hilo zitaendelea kutengwa.

Viongozi hao wamekubaliana kwa kauli moja kulisemea bara katika mustakabali wa changamoto mbalimbali ambazo bara hilo linakabiliana nazo kwa sasa ikiwemo matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi. Wamesema changamoto bado zinahitaji kiwango fulani cha usaidizi wa kimataifa kwa sababu hakuwezi kuwa na usalama wa afya duniani ikiwa Afrika itaendelea kuachwa.

Hayo yamesemwa jana Jumatatu  wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tano wa kimataifa wa Ajenda ya Afya Afrika (AHAIC) 2023 uliobeba ajenda kuu kuhusu hitaji la dharura la nchi za Kiafrika kuungana katika juhudi zao kuimarisha mifumo ya afya na kushughulikia changamoto za kiafya zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkutano huo umelenga kukusanya sauti za bara zima la Afrika kabla ya ushiriki wao katika kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 78) na kikao cha 28 cha Mkutano wa Nchi Wanachama (COP 28) kinachofanyika Septemba na Novemba mwaka huu.

Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Afrika cha Kkudhibiti magonjwa (Africa CDC) amesema, "Ingawa tunakubali kwamba nchi za Kiafrika lazima pia zichukue jukumu lao katika kuwekeza katika mifumo yao ya afya, lazima pia tutambue masuluhisho yanayoongozwa na Waafrika kwa Waafrika." 

Waziri wa Afya wa Rwanda, Dk Sabin Nsanzimana amesema  ikiwa bara linataka kushughulikia vitisho vinavyojitokeza katika makutano ya afya na mabadiliko ya hali ya hewa, nchi za Afrika lazima ziwasilishe msimamo mmoja katika kongamano la kimataifa la afya na hali ya hewa.

"Tunahitaji kuwa na ujumbe mmoja kwa Afrika moja tunapowasilisha maswali na madai yetu katika UNGA 78 na COP 28 kwa sababu ni hapo tu ndipo tunaweza kushawishi mabadiliko ya sera ya kimataifa yanayohitajika ili kukidhi mahitaji ya watu wa Afrika,” amesema.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, mamilioni ya watu wanasumbuliwa na umaskini mkubwa kutokana na kwamba, wanalazimika kulipia huduma za afya kwa kutumia karibu dola mbili kwa siku.