Jun 01, 2023 12:12 UTC
  • Kutishiwa kuwekewa vikwazo Uganda, njama za Marekani za kuzitwisha ufuska nchi za Afrika

Rais wa Marekani, Joe Biden amelaani sheria mpya iliyotiwa saini na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda dhidi ya vitendo vya ushoga na kusema kuwa Marekani inaweza kuiwekea Uganda vikwazo na ameitaka Uganda kufuta mara moja sheria hiyo.

Katika vitisho vyake hivyo, Biden ametishia kuangalia upya vipengee vyote vya uhusiano wa Marekani na Uganda. Ametoa vitisho pia vya kusimamisha misaada ya Marekani kwa Uganda na kuiwekea vikwazo vingi nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Amesema, serikali yake inafikiria kuchukua hatua zaidi dhidi ya Uganda kama kuzuia wahusika wa sheria hiyo kuingia nchini Marekani. Amedai kuwa eti sheria hiyo ni uvunjaji wa haki za binadamu. Naye Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje wa Marekani amesema, serikali ya nchi yake itaweka vikwazo vya visa dhidi ya viongozi wa Uganda. Waitifaki wa Washington huko barani Ulaya nao pia wametishia kuchukua hatua kama hizo dhidi ya Uganda. Josep Borrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema, hatua ya Uganda ya kupasisha sheria iliyo dhidi ya mashoga na watu wenye mahusiano haramu ya jinsia moja itaathiri uhusiano wa Kampala na washirika wake wa kimataifa. 

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Kwa mujibu wa sheria hiyo iliyotiwa saini na Rais Yoweri Museveni, watu wanaoshiriki kwenye vitendo vya liwati na usagaji watatumikia hadi kifungo cha maisha jela nchini Uganda. Rais Museveni alitia saini sheria hiyo Jumatatu wiki hii. Miongoni mwa vipengee vingine vya sheria hiyo ni adhabu ya kifo kwa wahalifu wakubwa wa ufuska huo. Lakini pia vipo vifungo vya miaka 10 na 20 mbali na vifungo vya maisha jela. Rais Museveni amewashukuru wabunge wa Uganda kwa hatua yao ya kishujaa na ya busara kubwa ya kupasisha sheria nzuri ya kupiga marufuku vitendo hivyo haramu. 

Lakini rais wa Marekani, Biden, amesema kuwa, ameliagiza Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya Marekani litathmini athari za sheria hiyo katika nyanja zote za ushirikiano wa nchi hiyo na Uganda, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa Marekani kusitisha kutoa huduma za usalama chini ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kusaidia maambukizi ya UKIMWI, (PEPFAR), na aina nyingine za msaada na uwekezaji. Vilevile rais huyo wa Marekani ameeleza kwamba, serikali yake itazingatia athari za sheria hiyo kama sehemu ya mapitio yake ya ustahiki wa Uganda wa kuwemo kwenye Sheria za Ukuaji na Fursa ya Afrika (AGOA). Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, mara nyingi hutumia silaha ya vikwazo dhidi ya nchi na mataifa yenye misimamo huru na yanayokhalifu sera za nchi hizo.

Endelea kusimama ngangari Uganda

 

Katika miongo ya hivi karibuni, nchi za Afrika zimekuwa kituo kikuu cha ugonjwa angamizi wa UKIMWI na umesababisha hasara kubwa za roho za watu na nguvu kazi pamoja na mifumo ya afya ya umma kwa nchi za Afrika. Watafiti wamegundua kuwa watu wenye mahusiano haramu ya jinsia moja na wanaojamiiana kinyume na maumbile ni sababu ya kuenea na kutomalizika maradhi na magonjwa hatari kwa wanadamu. Vitendo haramu vya ulawiti na usagaji ni haramu katika sheria rasmi za zaidi ya nchi 30 za  Afrika.

Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among alitangaza na kuthibitisha Jumatatu wiki hii kwamba, Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni amepasisha rasmi sheria ya kupiga marufuku uchafu huo nchini humo na kuwachukulia hatua kali wanaojihusisha na mahusiano ya kingono ya watu wa jinsia moja kwa mujibu wa Sura ya 91(3)(a) ya Katiba ya Uganda ya Mwaka 2015. Spika Among alisema: "Tumesimama kidete kulinda utamaduni, thamani na maazimio ya taifa letu, kwa mujibu wa malengo yetu ya taifa nambari 19 na 24, na pia kwa mujibu wa kanuni za sera zetu. Wananchi wa Uganda wamezungumza, na ni jukumu letu kuitelekeza sheria hii kwa uadilifu, kwa dhati na kwa njia madhubuti."

Kwa kweli vitisho vya rais wa Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Uganda vimetolewa katika hali ambayo Rais Yoweri Museveni kwa muda mrefu amekuwa mstari wa mbele kulaani vikali mahusiano haramu ya watu wa jinsia moja, na mwaka 2013 alitia saini sheria ya kukabiliana na ufuska huo licha ya mashinikizo na vitisho vya nchi za Magharibi.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa uganda akiwa ofisini kwake 

 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, moja ya sababu kuu ya kuendelea Marekani kutoa vitisho dhidi ya nchi huru duniani ni kulinda maslahi binafsi ya Washington na kuendeleza uistikbari wake duniani. Marekani ina ugonjwa wa uraibu wa kuweka vikwazo. Marekani imeziwekea vikwazo vya upande mmoja nchi nyingi duniani kama Iran, Russia, China, Venezuela, Cuba, Syria, Korea Kaskazini n.k. Tab'an madola ya Ulaya Magharibi nayo hayako nyuma katika kuifuata kibubusa Marekani. 

Sasa hivi Marekani imetishia kuiwekea vikwazo nchi huru ya Uganda kwa kisingizio cha kupasisha sheria ya kupiga marufuku uchafu wa maingiliano haramu ya jinsia moja. Juzi Jumanne, serikali ya Uganda ilijibu vitisho hivyo vya Marekani na kusema kuwa, wananchi wa Uganda hawaogopeshwi na vitisho hivyo. Jana Jumatano mamia ya wananchi wa Uganda waliandamana nchini humo kupinga vitisho vya Marekani na Ulaya na kuunga mkono viongozi wao katika suala hilo.  Naye Chris Baryomunsi, Waziri wa habari wa Uganda amesema: "Sisi hatuvihesabu vitendo vya liwati na usagaji kuwa ni haki ya mtu kisheria. Huo ni ufuska tu ambao sisi Waafrika na sisi Waganda hatuwezi kukubaliana nao kabisa. Ni sawa; tunapokea misaada kutoka nchi za Magharibi, lakini tunazikumbusha nchi hizo kwamba Uganda ni nchi huru na ina haki ya kujiwekea yenyewe sheria inazoziona ni sahihi kwake."

Tags