Jun 27, 2023 06:56 UTC
  • Afisa wa UN: Watu 600 wameuawa DRC ndani ya miezi 3

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa barani Afrika amesema kwa akali watu 600 wameuawa katika mashambulizi ya magenge yanayobeba silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Martha Pobee alisema hayo jana Jumatatu katika hotuba yake mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, mashambulizi hayo ya umwagaji damu yalifanywa na magenge ya waasi ya Cooperative for the Development of the Congo (CODECO), Zaire, na Allied Democratic Forces (ADF).

Ameeleza kuwa, hali ya usalama katika maeneo ya mashariki mwa DRC imezorota, licha ya kupungua mapigano baina ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Sanjari na kutoa mwito kwa makundi ya waasi na wabeba silaha kusitisha harakati zao za uasi mashariki mwa DRC, afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ametaka kutumwa tena vikosi vya serikali kurejesha utulivu katika maeneo hayo hasa mkoa wa Ituri.

Waasi wa M23

Alkhamisi iliyopita, Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa (NGOs) lilitangaza kuwa, watu 2,750 wameuawa katika majimbo yenye migogoro mikubwa mashariki mwa DRC ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Taarifa ya jukwaa hilo imesema uwepo wa makundi ya waasi wanaobeba silaha katika maeneo hayo ya mashariki mwa DRC umepelekea mamilioni ya wakazi kuyahama makazi yao, na hivyo kushadidisha hali mbaya ambayo inashuhudiwa katika maeneo hayo kwa miaka mingi sasa.

Tags