Iran: Israel ikomeshe ukaliaji ardhi za Wapalestina kwa mabavu
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na kusisitiza kuwa, mgogoro wa Palestina unaweza kupatiwa ufumbuzi tu kupitia kuhitimishwa ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na Wazayuni maghasibu.
Saeed Iravani amesema hayo katika hotuba yake katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokuwa kinajadili hali ya eneo la Asia Magharibi ikiwemo Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Iravani ameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dhati na za makusudi kukomesha ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Amezitaka jumuiya zote za kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama, ziwajibike kwa watu wa Palestina na kufanya jitihada za haraka ili kukomesha jinai za kila leo zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran vilevile amesisitiza uungaji mkono wa Iran kwa Wapalestina katika kuamua hatima yao wenyewe na kuunda nchi huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Baitul Muqaddas.
Kadhalika amelaani uamuzi wa serikali ya Israel yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu wa kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani kitendo cha walowezi wa Kizayuni cha kuvamia Msikiti wa Al-Aqsa, wakiongozwa na Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala haramu wa Israel.
Nasser Kan'ani amesema hatua hiyo ya walowezi wa Kizayuni wapatao 1,800 kushambulia Kibla hicho cha kwanza cha Waislamu na kuwazuia waumini wa Kipalestina kuingia kwenye Msikiti huo ni kitendo kingine cha kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu, kilichoumiza hisia za Waislamu kote duniani.