Iran yataka kusitishwa mapigano katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100664-iran_yataka_kusitishwa_mapigano_katika_kambi_ya_wakimbizi_wa_kipalestina_lebanon
Msemaji wa Wiziara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inatoa mwito wa kukomeshwa mapigano katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Ain Al-Hilweh nchini Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2023 04:27 UTC
  • Iran yataka kusitishwa mapigano katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina Lebanon

Msemaji wa Wiziara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inatoa mwito wa kukomeshwa mapigano katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Ain Al-Hilweh nchini Lebanon.

Nasser Kan'ani amesema kuna haja ya kusitishwa mapigano hayo yanayoendelea kwa siku kadhaa sasa, na yaliyopelekea kupoteza maisha na kujeruhiwa wakimbizi kadhaa wa Kipalestina.

Kan'ani amewakumbusha Wapalestina kuwa wanahitaji umoja na mshikamano wakati huu, kuliko wakati mwingine wowote ule.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran ameeleza bayana kuwa, pande zinazohasimiana kwenye mzozo huo zinapasa kusitisha mapigano, kudumisha utulivu na kukomesha uhasama baina yao.

Nasser Kan'ani amesema makundi, matabaka na harakati zote za Kipalestina zinapasa kuungana na kuelekeza nguvu na rasilimali zao katika kukabiliana na adui Mzayuni, ambaye ndio mzizi wa fitina na matatizo yote yanayolikumba taifa la Palestina.

Mapigano katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina Lebanon

Hii ni katika hali ambayo, utulivu wa kiwango fulani umeripotiwa kurejea katika kambi hiyo ya wakimbizi wa Kipalestina nchini Lebanon, kufuatia matamshi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrallah, ya kusisitizia ulazima wa kusitishwa mapigano katika kambi hiyo.

Kwa mujibu wa Dakta Riad Abu al-Einein, Mkuu wa Hospitali ya Al Hamshari katika mji wa pwani wa Sidon, watu 12 wameuawa na wengine karibu 60 wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo katika kambi ya Ain Al-Hilweh, ambayo kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, inahifadhi zaidi ya wakimbizi 63,000 wa Kipalestina.