Rais wa Iran: Biden amekiri kwamba Israel ni utawala bandia
-
Rais Ebrahim Raisi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran ameyataja matamshi yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Joe Biden, kuwa yanapinga maendeleo ya kisaisa na kijamii na demokrasia na ni dhidi ya binadamu na akasema: Matamshi ya hivi majuzi ya Rais wa Marekani ni kukiri bila hiari kwamba utawala ghasibu wa Israel ni utawala bandia.
Rais Ebrahim Raisi aliyasema haya jana mjini Tehran katika kikao cha baraza la mawaziri akijibu matamshi yaliyotolewa na Rais wa Marekani aliyesema kwamba, "lau utawala wa Kizayuni wa Israel usingekuwepo, Marekani ingefanya kazi kuuunda".
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hasira ya walimwengu na kuchukizwa kwao na jinai za kutisha zinazofanyika katika Ukanda wa Gaza, na kusema: "Leo walimwengu wanaziuliza serikali, madola yenye nguvu duniani na jumuiya za kimataifa kwamba, vipi wanaweza kuruhusu utawala dhalimu unaoungwa mkono na Marekani kuwaua wanawake na watoto wanaodhulumiwa wa Kipalestina huko Gaza kwa ukatili mkubwa mbele ya macho yao?
Amegusia pia uungaji mkono usio na aibu wa Marekani kwa uhalifu na jinai za Wazayuni, na kusema: Kauli iliyotolewa na Rais Joe Biden kwamba "kama kusingekuwapo utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia, Marekani ingefanya jitihada za kuuunda" inapinga maendeleo na mageuzi ya kisiasa na kijamii, demokrasia, na ni dhidi ya binadamu, na ina nukta kadhaa muhimu sana. Amesema kuwa: Nukta ya kwanza ni kwamba, Wamarekani wanapaswa kujibu, matamshi haya yanaoana na sheria, mkataba na kanuni gani za kimataifa?
Rais wa Iran amesema: Nukta ya pili muhimu katika matamshi hayo ya Joe Biden ni kwamba, matamshi hayo ni kukiri bila hiari kwamba utawala ghasibu wa Israel ni utawala bandia; na nukta ya tatu inayoweza kutambuliwa na serikali za nchi za Kiislamu kuwa ni onyo ni kwamba, matamshi hayo yanaeleza ukweli kwamba, kwa Marekani, kuulinda utawala ghasibu wa Israel ni muhimu zaidi kuliko maisha ya watu, hasa wanawake na watoto.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataja yanayojiri katika Ukanda wa Gaza dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa eneo hilo kuwa ni kielelezo cha wazi cha uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu, na amesisitiza udharura wa kuhukumiwa viongozi watendajinai wa Marekani na Israel ambao ndio wahusika wakuu wa uhalifu huo. Ameongeza kuwa: Damu iliyomwagwa kwa dhulma ya wananchi wanaikandamizwa wa Palestina itaharakisha anguko la utawala wa Kizayuni na kukombolewa Quds Tukufu.