Diplomasia yenye nguvu na amilifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Ghaza; tokea safari za kieneo hadi New York
(last modified 2023-10-28T07:55:32+00:00 )
Oct 28, 2023 07:55 UTC
  • Diplomasia yenye nguvu na amilifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Ghaza; tokea  safari za kieneo hadi  New York

Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika kuendelea na siasa za diplomasia amilifu na imara kuhusu Ghaza, amesafiri mjini New York ambapo ameshiriki katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza juu ya haja ya kuchukuliwa hatua muhimu za dharura ili kukomesha vita huko Ghaza

Hossein Amirabdollahian ni mmoja wa maafisa wa kigeni ambao wanajituma na kufanya jitihada nyingi kwa ajili ya kusimamishwa vita vya kikatili vinavyoendeshwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Ghaza.

Mara tu baada ya kuanza mashambulizi hayo, Amir Abdullahian alisafiri katika nchi nne ambazo ni Iraq, Lebanon, Syria na Qatar. Alishauriana na viongozi wa nchi hizo juu ya haja ya kusitisha vita dhidi ya Ghaza. Amir Abdollahian pia alihudhuria kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu mjini Jeddah, ambapo pamoja na kuzungumza katika kikao hicho, alishauriana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi kadhaa.

Wiki hii iliyopita, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa mwenyeji wa  Mawaziri wa Mambo ya Nje wa  Afrika Kusini na Niger, pamoja na Mawaziri 4 wa Mambo ya Nje wa Caucasus na Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Amir Abdollahian pia amekutana na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres huko mjini New York.

Ameshiriki katika kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Palestina huko mjini New York kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa muda wa Baraza la Usalama.

Amir Abdollahian amesisitiza katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ukweli ni kwamba uvamizi wa kinyama kwa kupita muda umebadilishwa kuwa ubaguzi mkubwa na wa kikatili.

Ni mchanganyiko huu wa ukaliaji mabavu na ubaguzi wa kupindukia wa muda mrefu ndio unaipa serikali katili ruhusa ya kisaikolojia ya kuwachinja na kuua kwa umati wananchi wasiokuwa na hatia wa Wapalestina.

Kwa hivyo, huu ni wakati mwafaka wa kutafakari na kuarifisha sura halisi ya ukatili wa utawala huo, kama lilivyofanya Baraza Kuu mwaka 1975 kupitia Azimio Namba 3379 kwa kubainisha 'Uzayuni kuwa ni ubaguzi wa rangi'.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa kinara katika kutetea haki za Palestina na hulichukulia suala la Palestina kuwa ni suala la Uislamu. Juhudi za kidiplomasia za Amir Abdullahian za kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni, kwa bahati mbaya zinakwamishwa na misimamo ya baadhi ya  nchi za eneo ambazo hadi sasa hazijaonyesha msimamo wowote thabiti na zimekaa kimya kuhusiana na jambo hilo. Hii leo, kwa upande mmoja, Ghaza inahitaji uungaji mkono wa nchi za Kiislamu ili kukomesha ukatili na jinai za utawala unaoukalia Quds kwa mabavu, na kwa upande mwingine, nchi za Kiislamu zinapasa angalau kutetea utambulisho wao wa kidini.

Mashambulizi ya jana usiku

Bila shaka moja ya sababu kuu za kiburi cha utawala wa Kizayuni katika kuendeleza mauaji yake ya umati dhidi ya wakazi wa Ghaza ni msimamo dhaifu wa nchi za Kiislamu. Hofu ya utawala wa Kizayuni ya kukabiliana na radiamali ya makundi ya Muqawama ni jambo muhimu linaloufanya utawala huo ujizuie kuanzisha vita vya nchi kavu dhidi ya Ghaza. Bila shaka, ikiwa nchi zote za Kiislamu zitafanya kama inavyofanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kujaribu kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni na kuushinikiza utawala huo dhalimu, Tel Aviv haitaweza kuendeleza tena vitendo vyake vya kuwaua kwa umati wananchi madhulumu wa Ghaza. Suala jingine muhimu ni kwamba, siasa za diplomasia amilifu na madhubuti za Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza zimefifisha madai na propaganda zinazojaribu kuonyesha kuwa Iran ndiyo inachochea hatua za Hamas dhidi ya utawala wa Kizayuni.

 

.

 

Tags