Iran: Mchakato wa kufuatilia jinai za Wazayuni kwenye duru za kimetaifa, umeanza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i104050-iran_mchakato_wa_kufuatilia_jinai_za_wazayuni_kwenye_duru_za_kimetaifa_umeanza
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria za kimataifa amesema kuwa, mchakato wa kufuatilia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza umeanza katika taasisi za kimataifa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 28, 2023 11:03 UTC
  • Iran: Mchakato wa kufuatilia jinai za Wazayuni kwenye duru za kimetaifa, umeanza

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria za kimataifa amesema kuwa, mchakato wa kufuatilia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza umeanza katika taasisi za kimataifa.

Jumamosi ya tarehe 7 Oktoba 2023, wanamapambano wa Palestina wakiongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya HAMAS walifanya operesheni ya kihistoria na ya kushtukiza ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa na kutoa pigo kubwa la kijeshi, kijasusi na kiusalama kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Operesheni hiyo ya kishujaa ilifanywa na wanamapambano wa Palestina kujibu jinai za makumi ya miaka za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Utawala pandikizi wa Israel ambao umeshindwa kupambana na wanamapambano wa Palestina kwenye medani ya mapambano, umeamua kufanya jinai kubwa kupindukia dhidi ya watoto, wanawake, vizee na watu wa kawaida huko Ghaza. 

Reza Najafi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya sheria za kimataifa amesema kwenye mahojiano yake na shirika la habari la IRNA kuhusu hatua zilizochukuliwa na Iran kuwasaidia kisheria Wapalestina kwamba, mbali na jitihada kubwa za kidiplomasia zinazoendelea kufanywa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran za kuutafutia ufumbuzi wa haraka mgogoro wa Ghaza na kukomeshwa mara moja mauaji ya kikatili yanayofanywa na Israel, mchakato wa kufuatilia jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina nao umeanza kwenye taasisi za kimataifa.

Reza Najafi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya sheria za kimataifa

 

Jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina ni kubwa mno kiasi kwamba, katika kipindi cha usiku mmoja wa kuamkia leo Jumamosi, wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni  wameua shahidi zaidi ya raia 100 wa Palestina.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa leo na Televisheni ya Al-Mayadeen, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu tarehe 7 Oktoba hadi leo Jumamosi imeongezeka na kufikia zaidi ya Wapalestina 7,400 huku 18,000 wengine wakijeruhiwa. 

Aidha vyombo vya habari vya Palestina vimesema kuwa, Wapalestina wapatao 100 wameuawa shahidi na kwa mkupuo mmoja katika shambulio la anga la jeshi katili la Israel dhidi ya jengo la makazi ya watu la Hayi al-Shati, magharibi mwa mji wa Ghaza. Watu wengi walikuwa wamekimbilia kwenye jengo hilo baada ya makazi yao kushambuliwa na kubomolewa kikatili na wanajeshi wa Israel.