Safari ya Waziri Mkuu wa Iraq Tehran wakati wa mgogoro wa Gaza
(last modified Tue, 07 Nov 2023 07:46:22 GMT )
Nov 07, 2023 07:46 UTC
  • Safari ya Waziri Mkuu wa Iraq Tehran wakati wa mgogoro wa Gaza

Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani, jana asubuhi akiwa ziarani hapa mjini Tehran alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Safari ya jana ya mjini Tehran ni ya tatu kufanywa na Shia al-Sudani akiwa Waziri Mkuu wa Iraq. Lakini kutokana na sababu kadhaa, ziara yake hiyo inatofautiana na ina umuhimu zaidi kulinganisha na zile zilizotangulia.

Ziara hiyo imefanywa saa chache tu baada ya safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani nchini Iraq. Jumapili usiku, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani mjini Baghdad. Kabla ya hapo, Blinken alikuwa ameelekea Jordan kushiriki mkutano wa Amman wa kujadili matukio ya Gaza uliohudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa baadhi ya nchi za Kiarabu. Na kabla ya Jordan, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alikuwa Tel Aviv, ikiwa ni safari yake ya pili aliyofanya huko tangu vilipoanza vita kati ya utawala wa Kizayuni na Hamas.

Blinken (kushoto) alipokutana na Waziri Mkuu wa Iraq Baghdad

Inavyoonekana, katika safari yake ya hapa mjini Tehran Shi'a al-Sudani atakuwa amebeba ujumbe wa salamu kutoka Marekani. Mwezi mmoja umepita tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza. Kwa kuzingatia kuwa Marekani inaziunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo, makundi ya muqawama ya Iraq nayo pia yameshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko nchini humo. Wamarekani wanaamini kuwa makundi ya muqawama ya Iraq yako chini ya ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na inavyoonekana, wamemtaka Waziri Mkuu wa Iraq aishawishi serikali ya Iran iyazuie makundi ya Iraq yasitishe mashambulio dhidi ya vituo vya Marekani, suala ambalo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalikataa kwa sababu kimsingi, Kimbunga cha Al-Aqsa kimeonyesha kuwa makundi ya Muqawama yako huru katika kujichukulia maamuzi.

Nukta nyingine ni kwamba, safari ya Shi'a Al-Sudani mjini Tehran imefanyika wakati wa maafa ya Gaza. Tangu mwezi mmoja uliopita, utawala haramu wa Kizayuni umekuwa ukiiandama Gaza kwa mashambulizi ya kinyama, kiasi kwamba hadi sasa watu wapatao 9,800 wameshauawa shahidi, ambapo zaidi ya 4,000 kati yao ni watoto. Serikali ya Iraq ni moja ya serikali za nchi za Kiarabu ambazo zimelaani rasmi jinai hizo za Wazayuni. Katika mkutano wa Cairo wa kujadili mgogoro wa Gaza, Waziri Mkuu wa Iraq alikuwa kiongozi pekee wa Kiarabu ambaye hakutumia neno Israel na alikosoa vikali vitendo vya kinyama vya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.

Jinai za kutisha na za kinyama za mauaji zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni Gaza 

Katika mazungumzo aliyofanya Waziri Mkuu wa Iraq na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, umetiliwa mkazo tena ulazima wa kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza katika kukabiliana na jinai za utawala unaoikalia Quds kwa mabavu. Katika mazungumzo na Shi'a Al-Sudani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei ameashiria hali ya kuhuzunisha ya Gaza na jinsi nyoyo za watu wote wenye fikra huru duniani zilivyosoneshwa na jinai na ukatili huo; na kwa mara nyingine tena akaeleza kwamba: "tangu siku za mwanzo kabisa za mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, ushahidi wote ulionyesha kuwa Wamarekani wanahusika moja kwa moja katika kuongoza vita, na kadiri vita hivi vinavyoendelea, sababu za kuhusika moja kwa moja Marekani katika kuongoza jinai za utawala wa Kizayuni zinazidi kupata nguvu na kudhihirika zaidi." Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongeza kuwa: "kama hakutakuwapo na msaada wa kijeshi na kisiasa wa Marekani, utawala wa Kizayuni hautaweza kuendelea kufanya kitu".

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu (kulia) na Waziri Mkuu wa Iraq

Waziri Mkuu wa Iraq yeye ameyataja mauaji ya kikatili ya Gaza kuwa ni sawa na kuwaadhibu na wasiohusika kwa watu wa eneo hilo dogo na akabainisha kwamba serikali na wananchi wa Iraq pamoja na mirengo ya kisiasa ya ndani ya nchi hiyo wako safu ya mbele ya uungaji mkono kwa watu wanaodhulumiwa wa eneo hilo; na serikali ya Iraq imefanya jitihada kubwa za kisiasa kwa lengo la kukomesha jinai za Gaza.

Nukta nyingine ni kwamba, Waziri Mkuu wa Iraq, kama walivyofanya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amekosoa mielekeo dhaifu ya unyamaziaji kimya inayoonyeshwa na jumuiya za kimataifa na uungaji mkono wa wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu kwa jinai zinazofanywa dhidi ya Gaza.

Kwa ujumla, ushirikiano uliopo kati ya Iran na Iraq katika masuala mbalimbali ya eneo ukiwemo mgogoro wa hivi sasa wa Gaza unaweza kuongeza uzito wa uungaji mkono kwa Muqawama dhidi ya wapinzani wake na wakati huo huo kuleta utulivu na usalama zaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia.../

 

Tags